KIJANA MMOJA mkazi wa Yombo Wilaya ya Temeke Hamza Kaisi amejikuta akiangukia katika mikono ya serikali baada ya Mahakama ya Wilaya ya Temeke kugundua kuwa anapaswa kutoa maelezo ya kujitetea baada ya kukamatwa na kete 70 na puli za bangi.
Uamuzi huo ulitolewa mwishoni mwa wiki hii na Hakimu Mkazi Mfawidhi Vicky Mwaikambo baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa Jamhuri.
"Baada ya kusikiliza ushahidi wote wa mashahidi wa Jamhuri, mahakama hii imebaini kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu. Atapanda kizimbani kujitetea Oktoba 15 mwaka huu," alisema Hakimu Vicky huku akimtazama mshtakiwa aliyekuwa ameinama kizimbani.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Nicas Kihuba, ulitoa ushahidi kupitia mashahidi wake akiwamo Koplo Abel Kusekwa, ambaye ndiye shahidi wa tano katika kesi hiyo.
Koplo Kusekwa alidai kuwa Julai 29, 2024 alipokea mshtakiwa Kaisi akiwa amekamatwa na mfuko mweusi uliokuwa na kete 70 na puli za bangi.
"Nilimpokea akiwa na mfuko huo nikafungua jalada la uchunguzi na kumkabidhi kwa mpelelezi Koplo Tumaini kwa hatua zaidi za kisheria," alidai.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa kuwa Julai 29, 2024 katika eneo la Yombo, Temeke, Hamza Kaisi alikamatwa na dawa hizo za kulevya kinyume cha sheria.
Mara baada ya uamuzi wa mahakama, Hamza alionekana mwenye wasiwasi lakini akitulia kusikiliza ratiba ya kesi yake kuendelea.