TARI yatoa mafunzo ya urushaji wa ndege nyuki za kilimo

Wizara ya Kilimo imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa mazao ikitoa mafunzo ya urushaji wa ndege nyuki za kilimo kwa wataalamu 16 yaliyofanyika tarehe 10 Octoba mwaka huu katika viwanja vya Nane Nane vya John Malecela, vilivyopo Nzuguni jijini Dodoma. 

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao wa Wizara ya Kilimo, Bi. Upendo Mndeme amewataka wataalamu kuhakikisha teknolojia hizo zinawafikia wakulima na kutatua changamoto zinazowakabili katika uzalishaji, ili kuongeza tija katika Sekta ya Kilimo.

Hivyo Bi. Mndeme amesema kupitia wataalamu hao Wizara ya Kilimo itaweza kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi ikiwatumia katika shughuli zote zinazohusu matumizi ya ndege nyuki za kilimo hasa katika maeneo yenye upungufu wa wataalamu na maeneo yote ya uzalishaji ikiwemo katika mashamba makubwa ya pamoja.

Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani kutoka Idara ya Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo. Bi. Justa Katunzi amesema matumizi ya ndege nyuki za kilimo yatarahisisha utoaji wa huduma za ugani ikiwemo upulizaji dawa katika mashamba pasipo kuathiri afya ya anayenyunyiza dawa hiyo tofauti na matumi ya teknolojia za hapo awali.

Aidha Bi. Eliada Muya ambaye ni Afisa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI)-Naliendele ni miongoni mwa watalaamu waliopata mafunzo hayo ambapo ameeleza kuwa matumizi ya ndege nyuki yatarahisisha shughuli za utafiti katika mazao mbalimbali ikiwemo zao la korosho hasa katika upande wa udhibiti wa visumbufu pamoja na matumizi ya mbolea za maji kwenye mikorosho.

Mafunzo yameshirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) pamoja na Bodi ya Korosho.

Matumizi ya ndege nyuki za kilimo yatarahisisha shughuli za utafiti, upimaji wa afya ya udongo, ufuatiliaji wa mashamba, matumizi ya viuatilifu na pembejeo hivyo kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uzalishaji.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii