Balozi wa Tanzania nchini Sweden Mhe. Balozi Mobhare Matinyi Oktoba 9 mwaka huu aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Biashara kati ya nchi za Nordic na Afrika uliofanyika jijini Oslo Norway.
Akifungua mkutano huo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Andreas Motzfeldt Kravik alieleza kuwa ni muhimu nchi za Nordic na Afrika ziwe na sera rafiki za pamoja za kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kwamba bara la Afrika linabeba mustakabali wa dunia.
Aidha Washiriki wa mkutano huo unaofanyika kila mwaka walitoka sekta binafsi, jumuiya za wafanyabiashara, viongozi wa serikali, wanadiplomasia na washiriki wengine kutoka asasi za nchi mbalimbali duniani ikiwemo Marekani.
Hivyo Kaulimbiu ya mkutano huo ilijikita katika kuhamasisha biashara, matumizi ya nishati safi, na ushirikiano wa kuimarisha miundombinu kati ya nchi za Nordic na Afrika.
Ujumbe wa Tanzania chini ya Balozi Matinyi ulimjumuisha pia Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Maua Matunda na Mbogamboga (TAHA) Jacqueline Mkindi na ulitumia fursa hiyo kutafuta masoko mapya ya bidhaa za Tanzania hususan kahawa, chai, korosho, vitunguu, viungo vya vyakula, maua na matunda.
Katika matumizi ya nishati safi Balozi Matinyi alifanya mazungumzo ya awali na kampuni za nishati za SCATEC iliyowakilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu Terje Pilskog ,RENERGY iliyowakilishwa na Afisa Uendeshaji Mkuu Mikkel Hansen, na CAMBI iliyowakilishwa na Meneja wa Mauzo wa Kanda ya Afrika Gary Brown.
Ujumbe wa Tanzania ulijikita pia kutafuta fursa za ushirikiano za kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa na majitaka kwa kuendeleza teknolojia bunifu za nishati safi, ambazo ni muhimu kwa mabadiliko ya mfumo wa nishati wa Tanzania; pamoja na fursa za kuendeleza mnyororo wa thamani kwenye sekta ya madini kupitia ujenzi wa miundombinu imara na rafiki kwa wachimbaji wadogo.