Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya chini ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamani Kuzaga amesema kielekea kilele cha mbio za mwenge wa uhuru ambao utahitimishwa kitaifa kesho oktoba 14 mwaka huu jijini Mbeya ulinzi umeimarishwa .
Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, Mwenge huo wa Uhuru uliingia mkoani humo Oktoba 7 mwaka huu ukitokea mkoa wa Songwe.
“Hadi sasa Mwenge umeshakimbizwa wilaya zote tano na halmashauri saba na kote huko hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa kwa ushirikiano wa wananchi Jeshi la Polisi na wadau mbalimbali,” amesema Kamanda Kuzaga.
Amesema Oktoba 14 mwaka huu mbio hizo zitahitimishwa rasmi jijini Mbeya tukio ambalo pia litaambatana na maadhimisho ya kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Amesema wageni wa kitaifa wamewasili jijini Mbeya viongozi wa kitaifa wakitarajiwa kuungana nao katika kilele cha maadhimisho hayo.
Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kudumisha utulivu na amani wakati wa shughuli hizo pamoja na kufuata sheria za usalama barabarani.
“Tunawaomba watumiaji wa barabara wazingatie maelekezo ya askari, ili kuruhusu misafara kupita salama.
Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha ulinzi unaendelea kuimarika wakati wote wa shughuli za kuzimwa Mwenge wa Uhuru na baada ya hayo hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayekiuka sheria kwa makusudi wakati wa maadhimisho hayo.