Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya
Rushwa na Uhujumu Uchumi imesema Ijumaa Februari 18, 2022 itatoa uamuzi
iwapo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wana kesi
ya kujibu au la katika kesi ya ugaidi inayowakabili.
Jaji Joachim
Tiganga anayesikiliza kesi hiyo amesema hayo jana Jumanne Februari 15,
2022 baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahaka kuwa wamefunga kesi
hiyo kwa shahidi wa 13 kuhitimisha ushahidi wake.
Shahidi huyo wa
13 wa upande wa mashtaka ambaye ni Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya
Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila alimaliza
kutoa ushahidi baada ya kuhojiwa maswali ya dodoso na upande wa utetezi.
Baada
ya shahidi huyo kuhitimisha ushahidi wake, Wakili wa Serikali Robert
Kidando aliiambia Mahakama kuwa wamefunga ushahidi na kuiomba ione kuwa
washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.
“Baada ya ushahidi wa
shahidi huyu wa kumi na tatu tunaialika Mahakama yako chini ya kifungu
41 (1) cha sheria ya Uhujumu Uchumi ione washtakiwa wote wanne wana kesi
ya kujibu hivyo hatua nyingine kwaajili ya kujitetea ifuate kwa upande
wetu tunafunga kesi hii” alisema Wakili Kidando
Hata hivyo, baada
ya upande wa mashtaka kutoa ombe hilo, upande wa utetezi kupitia Wakili
Peter Kibatala uliomba kupewa nafasi ya kufanya mawasiliano ya mdomo
pamoja na kupewa mwenendo wa kesi.