Kijana aliyepigwa picha akipika jangwani apata msaada

Mwandishi wa habari wa Ethiopia aliyepiga picha ya mvulana akipika jangwani peke yake ilyosambaa kwenye mitandao ya kijamii amezungumzia kisa cha picha hiyo yenye ujumbe mzito.

Picha ya Boru Konso imezua hisia nyingi mtandaoni na kupata watu waliojitolea kumchangia pesa na vitu vingine mvulana huyo.

Mwanahabari huyo alikuwa akiendesha pikipiki yake katika wilaya ya mashambani ya Mio ambako alikuwa ameenda kuandika habari alipomwona mvulana huyo jioni sana.

"Mvulana huyo mdogo ambaye pengine umri wake ni chini ya miaka 10, alikuwa amewasha moto na anapika chakula. Nilishtuka nilipomwona mtoto huyu akipika jangwani akiwa peke yake. Huwezi kuona nyumba katika eneo hilo kwa karibu kilomita 10. Niliegesha pikipiki yangu na kumpiga picha," Boru anasema.

Mvulana huyo alimwambia mwandishi wa habari kwamba familia yake inaishi katika wilaya tofauti na alikuwa akizunguka na wanyama wao kutafuta maji na malisho.

Ethiopia kwa sasa inakabiliwa na ukame unaowalazimu wafugaji kuzunguka kutafuta malisho.

Boru alishiriki picha ya mvulana huyo kwenye mitandao ya kijamii na watu wakaanza kuwasiliana ili kutoa msaada.

Miongoni mwa waliomtembelea kijana huyo ni mfanyabiashara Muna Bakare ambaye alitoa msaada wa vyakula na vitu vingine kwa kijana huyo, familia yake na majirani.

"Niliiona kwenye mitandao ya kijamii picha ya mtoto huyu mdogo ikagusa moyo wangu, sikupata usingizi kabisa, nilihisi kama ni mwanangu, nikaanza kumtafuta," Muna alisema.

Muna ameahidi kumlipia mtoto huyo ada ya shule hadi atakapomaliza chuo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii