Kesi ya wakili wa Kenya kuanza katika mahakama ya ICC

Kesi ya wakili wa Kenya anayetuhumiwa kuwahonga mashahidi wa upande wa mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC) inaanza Jumanne huko The Hague.

Paul Gicheru anakabiliwa na mashtaka ya kuzuia kutendeka kwa haki kwa kuwashawishi mashahidi kwa ufisadi kuhusu kesi za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/2008 nchini Kenya.

Alijisalimisha mwenyewe kwa mahakama mnamo mwezi Novemba 2020.

Miaka mitano baada ya mahakama ya ICC kutoa hati ya kukamatwa kwake, wakili Mkenya Paul Gicheru kesi yake inaanza kusikilizwa huko The Hague, akituhumiwa kuhujumu kesi ya mahakama inayohusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007.

Waendesha mashtaka wanadai kuwa alishawishi mashahidi kwa rushwa na kudhoofisha kesi hiyo. ambayo ilimkabili Naibu Rais wa sasa William Ruto.

Waendesha mashtaka wanadai kuwa alishawishi mashahidi kwa ufisadi na kuhujumu kesi iliyokuwa ikimkabili Naibu Rais wa sasa William Ruto.

Ruto alikabiliwa na mashtaka ya mauaji, uhamisho na mateso wakati wa ghasia zilizofuatia uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo takriban watu 1,200 waliuawa.

Hata hivyo, Bw Ruto amekuwa akikana mashtaka kila mara.

Mahakama ya ICC ilitupilia mbali kesi dhidi ya Ruto ikitaja ukosefu wa ushahidi lakini ikakataa kumwachilia huru.

Majaji walisema kumekuwa na uingiliaji kati wa mashahidi na uingiliaji wa kisiasa katika kesi hiyo.

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa rais wa kwanza wa nchi kufika katika mahakama ya ICC huko The Hague mwaka wa 2014, lakini mashtaka dhidi yake na wengine watatu yalitupiliwa mbali baadaye mwaka huo huo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii