Hospitali ya Benjamin Mkapa
imefanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 26 kuanzia machi 22, 2018 kutoka
mikoa mbalimbali nchini na wote wanaendelea vizuri.
Hayo
yamebainishwa leo na Mkuu wa idara ya Magonjwa ya Figo Dkt. Anthony
Gyunda hospitali ya Benjamini ameeleza kuwa "Uharibifu
wa Figo unasababishwa na taka sumu pamoja na magonjwa yote yanayoathiri
mwili kama kisukari, shinikizo la damu na presha pamoja na magonjwa
yanayoambukiza na yasiyoambukiza." amesema Dkt. Gyunda
"Kuna
hatua tano za matibabu ukigundulika na ugonjwa wa Figo ikiwepo hatua ya
haraka ambayo ni uchujaji wa damu na hatua ya mwisho ni upandikizaji wa
figo."amesema Dkt. Gyunda
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Figo Dkt.Anthony Gyunda akielezea huduma za
magonjwa ya Figo zinavyotolewa kwenye hospitali ya Benjamin Mkapa
iliyoko jijini Dodoma.
Aidha, Dkt. Gyunda ametoa ushauri
kwa wananchi kuepuka matumizi ya ulaji wa nyama kwa wingi, utumiaji wa
sukari, mafuta ya kula pamoja na unywaji wa pombe ili kuepuka Magonjwa
yasiyokuwa ya lazima ikiwemo ugonjwa wa figo.
"Epukeni matumizi
holela ya dawa, nendeni mkapate vipimo na ushauri wa wataalamu kwakuwa
matumizi ya Dawa kiholela sio mazuri kiafya na hii hupelekea kuua mfumo
wa Figo."amesema Dkt. Gyunda
Hivyo basi, Dkt. Gyunda amewasihi
wananchi kupata vipimo kila mara, angalau mara mbili kwa mwaka ili kujua
Afya zao na kuepuka gharama za matibabu.
Dkt. Gyunda amesema
katika hospitali hiyo wanapokea wagonjwa mbalimbali kutoka Mikoa jirani
ikiwemo Iringa, Singida, Manyara na Mikoa mengine.
Pia ameishukuru Serikali kupitia wizara ya Afya kwa kuwawezesha upatikanaji wa watumishi wenye weledi pamoja na vifaa tiba.
Mmoja
wa wagonjwa katika kitengo cha Figo ambaye ni kijana mwenye mwenye umri
wa miaka 17 amesema anapata matibabu ya uchujaji wa Damu katika
hospitali hiyo na anaendelea vizuri.
Kwa upande wake mtaalamu wa
Magonjwa ya uti wa mgongo Dkt. Waziri Jimmy amesema sio lazima kila
tatizo kufanyiwa upasuaji Magonjwa mengine yanaisha kwa kutumia dawa.
"Ili
kujua tatizo mapema lazima kupata vipimo kwa kuwaona Wataalamu kabla
ugonjwa haujazidi hadi kupelekea kufanyiwa upasuaji." amesema Dkt. Jimmy
Mara nyingi magonjwa yasiyoambukiza hayana dalili hivyo ni
muhimu kujua Afya yako kabla ya tatizo kujitokeza, afadhali kutumia
gharama za vipimo kuliko kutumia gharama za matibabu.