Mgomo wa walimu waingia wiki ya pili

Mgomo wa walimu ambao umeathiri taasisi za elimu nchini Zimbabwe umeingia wiki yake ya pili jana Jumatatu.

Serikali imewasimamisha kwa muda walimu wapatao 135,000 kwa kushindwa kuripoti kazini. Wizara ya elimu ilitangaza kuwasimamisha walimu wiki iliyopita ikidai kuwa adhabu hiyo itadumu kwa miezi mitatu.

Walimu wengi walishindwa kufika kazini wakidai kuwa hawawezi kumudu gharama za usafiri kufika ofisini. Baadhi ya shule zilikuwa tupu, zikiwa hazina walimu wala wanafunzi na nyingine wanafunzi wameshuhudiwa wakifika darasani bila ya uwepo wa walimu.

Serikali na walimu wamekuwa wakitofautiana kuhusu malipo kwa muda miaka mitatu sasa. Serikali iliacha kuwalipa walimu mishahara kwa dola ya Kimarekani na badala yake ikaanza kuwalipa kwa Dola ya Zimbabwe. Mabadiliko hayo yaliwaathiri walimu kutokana na mfumuko wa bei.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii