MAHAKAMA Kuu ya Kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) inatarajiwa leo kutoa uamuzi wa kwanza kuhusu mashtaka yanayomkabili Rais wa zamani, Joseph Kabila Kabange, akihusishwa na vuguvugu la waasi la M23.
Mwezi uliopita, upande wa mashtaka uliomba mahakama imhukumu adhabu ya kifo na kuamuru kukamatwa kwa mali zake. Kabila anakabiliwa na mashtaka ya uhaini, kushirikiana na magaidi na kuunga mkono ugaidi.
Hata hivyo, Rais huyo wa zamani Joseph Kabila hajawahi kufika mahakamani na anatarajiwa kutokuwepo pia wakati wa hukumu. Kupitia vyombo vya habari, Kabila aliita mashtaka hayo ni propaganda za kisiasa unaolenga kuficha udhaifu wa serikali ya sasa.
Iwapo atapatikana na hatia, Kabila atakuwa rais wa kwanza wa zamani wa DRC kuhukumiwa na mahakama tangu kuondoka madarakani.