TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imethibitisha wagombea 11 wa urais wa Zanzibar kati ya 17 waliochukua fomu za uteuzi, baada ya kukidhi vigezo vya kisheria vilivyowekwa.
Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi, alitangaza majina ya wagombea hao katika hafla ya ugawaji vyeti iliyofanyika Makao Makuu ya tume Maisara, na kusema kuwa kila mgombea atapewa gari jipya, dereva na mlinzi kwa ajili ya kampeni, huku tume ikibeba gharama zote za mafuta na matengenezo.
“Tunataka kuhakikisha kila mgombea ana mazingira sawa ya kufanya kampeni kwa haki, huru na usalama. Baada ya uchaguzi gari hizo zitarejeshwa,” alisema Jaji Kazi.
Miongoni mwa walioteuliwa ni: Dk. Hussein Ali Mwinyi (CCM), Othman Masoud Othman (ACT Wazalendo), Juma Ali Khatib (ADA Tadea), Hamad Ibrahim Mohamed (UPDP), Ameir Hassan Ameir (Chama cha Makini), Said Soud (AAFP), na Bi Lela Rajab Khamis (NCCR-Mageuzi). Wengine ni Hassan Juma Salum (TLP), Khamis Faki Mgau (NRA), Hamad Rashid (ADC), na Mfaume Khamis Hassan (NLD).
Walioenguliwa
Jaji Kazi amesema kati ya wagombea 17 waliochukua fomu, watano hawakuzirejesha huku mgombea mmoja wa CUF akikataliwa baada ya kushindwa kukidhi vigezo. Vyama vilivyoshindwa kurejesha fomu ni CCK, DP, SAU, UMD na UDP. Aidha, licha ya changamoto za udhamini, mgombea wa ACT-Wazalendo alithibitishwa baada ya tume kubaini kuwa alipata idadi ya chini inayokubalika kisheria katika kila mkoa. Kampeni zaanza rasmi
Baada ya kutangazwa rasmi, wagombea hao walikabidhiwa vyeti vya uteuzi kwa mujibu wa kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Uchaguzi Na. 4 ya mwaka 2018, na kuruhusiwa kuanza kampeni kuanzia saa 12 jioni ya Septemba 11 mwaka huu.
Mwenyekiti wa ZEC aliwapongeza vyama vya siasa kwa ushirikiano waliouonesha tangu mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu, na akawataka wagombea kuendesha kampeni za kistaarabu, zenye kuzingatia amani, maadili ya uchaguzi na utu wa Wazanzibari. “Tume itaendelea kusimamia kwa karibu shughuli zote za uchaguzi ili kuhakikisha wananchi wanapata viongozi waliochaguliwa kwa haki na uwazi,” alisisitiza.