SERIKALI ya China imesema itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha taifa linapiga hatua za haraka kwenye maendeleo ya kiuchumi yanayochochewa na teknolojia ya kidijitali.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa China nchini, Chen Mingjian, wakati wa hafla ya kuwapongeza washindi wa mashindano ya kimataifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa mwaka 2024/25, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Katika mashindano hayo yaliyoshirikisha nchi 48, Tanzania iliibuka mshindi wa kwanza duniani katika eneo la Cloud na kushika nafasi ya pili kwenye kiwango cha dunia katika eneo la Network. “Serikali ya China imedhamiria kuhakikisha Tanzania inafanikisha maendeleo ya kidijitali yatakayochochea ukuaji wa uchumi kwa kasi kubwa,” alisema Balozi Chen.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Amos Nungu, alisema ushindi huo ni hatua kubwa kwa taifa. “Ushindi huu unaifanya Tanzania kuwa na nafasi bora ya kujenga rasilimali watu wenye ujuzi wa uhakika katika TEHAMA, watakaosukuma gurudumu la maendeleo ya kiuchumi kwa kasi zaidi,” alisema Dk. Nungu. Hafla hiyo pia ilihusisha uzinduzi wa msimu mpya wa mashindano ya vipaji vya TEHAMA kwa mwaka 2025/26, yatakayofanyika nchini China.