Wagombea wote watakiwa kuwasilisha gharama za kampeni kabla ya siku husika kufika

Wagombea wa nafasi za Rais, Wabunge na Madiwani katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 wametakiwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Uchaguzi, ikiwemo kuwasilisha taarifa za gharama za kampeni kabla ya siku ya uteuzi, vinginevyo wanaweza kuwekewa pingamizi la kugombea.

Hayo yamesemwa na CPA Edmund Mugasha, Mkuu wa Sehemu ya Ruzuku katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, wakati wa Mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa Viongozi wa Kitaifa wa Vyama vya Siasa yaliyofanyika  Agosti 18, 2025 kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

“Kifungu cha tatu cha Sheria ya Uchaguzi kinampa nguvu Msajili wa Vyama vya Siasa kuweka pingamizi kwa mgombea yeyote aliyeteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi iwapo hajawasilisha taarifa za gharama za uchaguzi. Hii ni kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria ambayo sasa yanataka gharama zielezwe kabla ya siku ya uteuzi,” amesema CPA Mugasha.

Amebainisha kuwa tayari Ofisi ya Msajili imesambaza fomu za kutangaza gharama za uchaguzi katika kata zote 3,960 za Tanzania, majimbo yote 272 ya Tanzania Bara na majimbo 50 ya Zanzibar, ambapo wagombea wanatakiwa kuchukua na kurejesha fomu hizo kwa mujibu wa sheria.

“Msajili anaweza kuweka pingamizi siyo tu kwa mgombea asiyewasilisha gharama, bali pia kwa yeyote atakayehusishwa na vitendo vinavyokatazwa kisheria wakati wa uchaguzi,” ameongeza.

Mafunzo hayo yamewaleta pamoja viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa na wadau mbalimbali kwa lengo la kuwaongezea uelewa juu ya utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ili kuepusha dosari wakati wa kampeni na uchaguzi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii