Chama cha Mapinduzi (CCM) leo kinatarajia kushuhudia tukio kubwa la kisiasa baada ya msemaji maarufu wa michezo na kada wa chama hicho, @hajismanara,kuchukua rasmi fomu ya kugombea nafasi ya Udiwani katika Kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Zoezi la uchukuaji fomu litafanyika katika Ofisi za Mtendaji Kata ya Kariakoo, ambapo mtendaji ndiye Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, zilizopo eneo la Arnatogolo Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Hatua hii ni mwendelezo wa mchakato wa kidemokrasia ndani ya chama, baada ya Manara kuibuka mshindi katika kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni na kuthibitishwa na vikao halali vya CCM, hivyo kupata ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa, shamrashamra za tukio hilo zitaanza mapema leo asubuhi katika Mtaa wa Mzizima/Mafia, zikihusisha msafara wa wanachama na wapenzi wa CCM.
Msafara huo utapita katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo ikiwemo Livingstone na kuendelea hadi Agrey, kabla ya kuishia katika Mtaa wa Lumumba kwa mapokezi ya kisherehe.
Baada ya hapo, msafara utaelekea katika Ofisi za CCM Kata ya Kariakoo zilizopo Mtaa wa Sikukuu, kwa ajili ya shughuli za ndani za chama na kuhitimisha rasmi zoezi la siku hiyo.