Wagombea wahimizwa kufuata Sheria za uchaguzi

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi, amewataka viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa kutumia nafasi ya mafunzo ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa umakini ili wawe walimu bora na wasaidizi kwa wagombea na viongozi wa chama katika ngazi za chini.

Akizungumza  Agosti 18 mwaka huu wakati akifungua mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), mkoani Dar es Salaam, Jaji Mutungi amesema kikao hicho kimeandaliwa kwa siku moja pekee ili kuwapa nafasi viongozi kuendelea na ratiba zao za maandalizi ya uchaguzi, ikiwemo mchakato wa uteuzi na upatikanaji wa wadhamini.

“Ninatambua kwamba hivi sasa mpo kwenye michakato ya uteuzi wa wagombea na kutafuta wadhamini. Hivyo nikaona nifanye nanyi kikao hiki cha siku moja pekee, muweze kuendelea na majukumu yenu muhimu ya maandalizi ya uchaguzi,” amesema Jaji Mutungi.

Amesisitiza kuwa vyama vya siasa haviwezi kuepuka jukumu la kushiriki uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kwani wagombea wote lazima wadhaminiwe na vyama.

“Kikao cha leo ni sehemu ya maandalizi hayo. Tofauti yake ni kwamba leo mtafundishwa namna ya kuzingatia kwa ukamilifu matakwa ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Mafunzo haya yamekusudia kuwaongezea uelewa ili mkatekeleze matakwa hayo ya kisheria,” amesisitiza.

Aidha, amewataka viongozi waliopata mafunzo hayo kuyatumia ipasavyo kwa ajili ya kuelimisha wagombea, viongozi wa chama na mawakala katika ngazi zote kuanzia wilaya, majimbo hadi kata.

“Wito wangu ni kwamba mtumie fursa hii vizuri ili mkawe walimu au wakala wazuri kwa wagombea na viongozi wenu wa ngazi za chini. Sikilizeni kwa makini maelezo na maelekezo mtakayopatiwa na watendaji na myafanyie kazi,” amesema Jaji Mutungi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii