Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim
Hamis Juma amefunga kikao kazi cha Majaji Wafawidhi mwishoni mwa wiki
iliyopita tarehe 11 Februari, 2022 huku akitoa rai kwa Majaji hao
kutekeleza na kueneza mazuri yote waliyoyapata katika kikao hicho ili
kuboresha zaidi huduma ya upatikanaji haki kwa wananchi.
Akizungumza
na Waheshimiwa Majaji Wafawidhi katika Ukumbi wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) uliopo jijini Arusha, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma amesema
kuwa ili kwenda pamoja ni vyema kuwashirikisha Watumishi wa Mahakama wa
ngazi mbalimbali pamoja na Wadau ili kuimba wimbo mmoja wa kuboresha
huduma za Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim
Hamis Juma akizungumza na Wahe. Majaji Wafawidhi (hawapo katika picha)
wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha Majaji hao kilichoanza
tarehe 10 Februari, 2022 katika Ukumbi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) jijini Arusha.
“Sisi ni kama Mabalozi na pia ni wawakilishi
wa wale ambao tunaowaongoza, hayo mazuri ambayo tumeyapata hapa
tuhakikishe tunayafikisha kwa njia mbalimbali na mimi naamini baada ya
ninyi kupitia tanuri ya mkutano huu mtakuwa ni viongozi bora kuliko
mlivyokuwa kabla ya kuanza kwa mkutano kwa sababu mmepata mada
mbalimbali zenye manufaa makubwa katika utendaji kazi,” alisema Jaji
Mkuu.
Aliongeza kwa kuwataka Majaji hao kuwa na desturi ya
kujisomea zaidi kwakuwa dunia ya sasa ina mambo mengi ya kimaboresho
hivyo kujisomea kutawezesha kupata taarifa nyingi zaidi ambazo zitakuwa
za manufaa katika uboreshaji wa huduma za kimahakama.
Naye, Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani
amewasisitiza Majaji hao kuzingatia masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na
kuimarisha matumizi ya mfumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa kuratibu
mashauri kwa njia ya Kielektroniki (JSDS II).
“Wahe. Majaji
tunakwenda kwenye Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’, safari imeanza na sio
jukumu la Mhe. Jaji Mkuu pekee, Majaji Wafawidhi ndio wasimamizi wa
kuwezesha hili, hivyo tusilege kutumia mifumo iliyopo ili kufikia azma
yetu,” amesema Mhe. Siyani.
Amesisitiza pia kuhusu matumizi ya
teknolojia katika kusikiliza mashauri hususani matumizi ya ‘Video
Conference’ ambapo amesema kila mmoja ahakikishe kuwa teknolojia
inatumika kwa kiasi kikubwa kwakuwa ni suala linalowezekana hivyo
linahitaji uamuzi na utayari wa wote.
Hali kadhalika, Mhe. Jaji
Siyani amewakumbusha Wahe. Majaji Wafawidhi kusimamia vyema utendaji
kazi wa Mahakama za chini ambazo ni Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Hakimu
Mkazi kwenye kuongeza kasi ya uondoshaji wa mashauri.
“Tusimamie
vyema Mahakama za Mwanzo na zote zilizopo chini yenu ili kasi ya
uondoshaji wa mashauri iendelee, Mahakama hizo ndio zinazojenga taswira
ya Mahakama kulingana na ukweli kwamba zinapokea idadi kubwa ya
mashauri,” alisisitiza Jaji Kiongozi.
Katika siku ya pili ya
Kikao kazi hicho Mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo; mada ya Hali ya
Mashauri na Mikakati yake iliyowasilishwa na Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma ambapo katika mada yake aliainisha
mafanikio kadhaa ikiwemo kukamilika kwa uandaaji wa Taarifa ya Utendaji
Kazi za Mahakama ya Tanzania kwa mwaka 2021 ‘Comprehensive Performance
Report of the Judicial Functions 2021’.
Mada zingine ni hali ya
mlundikano na Mikakati ya Kanda/Divisheni kuondoa mlundikano
iliyowasilishwa na Majaji Wafawidhi, Dhana ya Vituo Jumuishi, ukaguzi wa
Mahakama na nyingine.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mshauri,
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha akiwaonyesha Majaji
Wafawidhi (hawao katika picha) moja ya nakala ya kitabu cha Taarifa ya
Utendaji Kazi za Mahakama ya Tanzania kwa mwaka 2021 ‘Comprehensive
Performance Report of the Judicial Functions 2021’.
Miongoni mwa maazimio ya kikao hicho
kilichoanza tarehe 10 Februari, 2022 ni Mahakama kufanya mawasiliano na
Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) na vyuo vingine vinavyotoa mafunzo ya
utunzaji wa kumbukumbu ili kuanzisha Mitaala ya mafunzo ya utunzaji wa
kumbukumbu kielektroniki ili iendane na mabadiliko/uboreshaji wa
matumizi ya TEHAMA yanayoendelea mahakamani na katika sekta nyingine.