Takukuru Tarime yamkamatwa masaidizi wa Mbunge mstaafu

Elisha Samo ambaye ni Katibu wa Mbunge mstaafu wa Jimbo la Tarime Mjini, Mhe. Michael Mwita Kembaki, anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Tarime kwa tuhuma za kuendesha mikutano ya kisiasa kinyume na taratibu za Chama Cha Mapinduzi CCM. 

Inadaiwa kuwa mikutano hiyo haikufuata mwongozo rasmi uliotolewa na Katibu Mkuu wa chama, hali inayotafsiriwa kama ukiukaji wa kanuni za chama na utovu wa nidhamu kwa mujibu wa taratibu za kisiasa ndani ya CCM.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizotolewa na Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Tarime Hery Mchume, hatua ya kumkamata msaidizi huyo wa Mwita Kembaki ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusiana na tuhuma za kuwakusanya wajumbe wanaotarajiwa kupiga kura za maoni hapo kesho kwa ajili ya kuwagawia rushwa kuwashawishi kumpigia kura Michael Kembaki anayewania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi kugombea Ubunge Jimbo la Tarime Mjini. 

Akizungumza na vyombo vya habari Kamanda Mchume alithibitisha kuwa uchunguzi huo unalenga kubaini kiwango cha ukiukwaji wa taratibu pamoja na iwapo kulikuwa na matumizi mabaya ya nafasi ya kisiasa aliyonayo mhusika.

Alipoulizwa kuhusu kiwango cha fedha ambacho amekamatwa nacho Msaidizi huyo wa Michael Kembaki, kamanda Mchume amesema kuhusu fedha taarifa itatolewa baada ya uchunguzi kukamilika kwani bado wanaendelea na mahojiano huku akiahidi kutoa taarifa kamili kuhusu sakata hilo,

Kwa upande mwingine TAKUKURU Wilaya ya Tarime imetoa wito kwa wagombea kufuata kanuni za Uchaguzi na kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii