WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa
amesema wataendeleza ushirikiano na Wizara ya Kilimo ili kuhakikisha
kuwa wanaimarisha Sekta ya Kilimo nchini.
Mheshimiwa Waziri
Bashungwa ameyasema hayo Februari 8,2022 jijini Dodoma wakati wa kikao
cha pamoja na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe pamoja na wakuu wa
mikoa yote Tanzania Bara kujadili namna bora ya kuboresha kilimo.
Waziri
Bashungwa amesema, "wakati sasa umefika wa kuhakikisha kuwa
tunaunganisha mahitaji yetu na yale ya Wizara ya Kilimo kwa kuhakikisha
kuwa bajeti inakua jumuishi na ya kutosha kutatua changamoto
zinazokabili Sekta ya Kilimo kwenye Tawala za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa,"amesema.
Amesema, "hata ile mikopo yetu tunayoitoa kwenye halmashauri ya asilimia 10 iangalie namna ya kusaidia vikundi vya kilimo
vinavyolima kisasa kwa kuvipatia mikopo ili waweze kuboresha kilimo chao,"ameongeza Mheshimiwa Bashungwa.
Naye
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema wizara yake ipo tayari
kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Rais-TAMISEMI ili kuhakikisha Sekta
ya Kilimo inaleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Hatuwezi
kufanikiwa katika kilimo kama hatutashirikiana na Ofisi ya
Rais-TAMISEMI katika mipango yetu ndio maana leo nimeona ni vyema kuja
kukutana na wakuu wa mikoa moja kwa moja na vikao viendee hata kila
baada ya miezi mitatu ili tuweze kupeana mrejesho na kupanga mipango ya
baadae ya utekelezaji,"amesema Mheshimiwa Bashe.
Amesema, maeneo
makubwa ambayo wataendelea kuyaangalia katika vikao hivi ni pamoja na
huduma za ugani, kilimo na umwagiliaji na ujenzi wa maghala ya kisasa ya
kuhifadhia mazao.
Pia amebainisha eneo lingine muhimu katika
kuimairisha kilimo kuwa ni mfumo wa stakabadhi ghalani, upatikani wa
mbolea ya uhakika kukomesha rumbesa katika uuzaji wa mazao kwa kuanzisha
vituo vya masoko vijijini na kutoa miongozo inayosimamia uuzaji wa
mazao ya wakulima.