IMEELEZWA lengo la kufikia 50 kwa
50 katika uongozi na nafasi za kufanya maamuzi nchini litafanikiwa tu
endapo wanawake zaidi wataendelea kupata nafasi za uongozi kuanzia
katika vyama vya siasa, mashirika na taasisi mbalimbali zikiwemo za
umma.
Hayo
yameelezwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake
katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF) Anna Kulaya wakati wa
mkutano uliowakutanisha wadau wa masuala yanayohusu Wanawake pamoja na
viongozi wa vyama vya siasa.
Kulaya
amefafanua kwa sasa Tanzania ni wazi imepiga hatua kubwa katika
kumkomboa mwanamke kiasi cha kuwa na Rais mwanamke ambaye ni Mama Samia
Suluhu Hassan lakini hiyo haimaanishi ndio iwe mwisho wa kuendelea
kumpigia mwanamke katika nafasi za maamuzi.Hivyo amesisitiza 50 kwa 50
itafikiwa endapo wanawake zaidi wataendelea kuaminiwa na kupewa nafasi.
"Sote
tunafahamu mlango mkubwa ambao umekuwa ukiwawezesha wanawake kuwa
katika nafasi za maamuzi ni siasa ambako huko wanapatikana wabunge,
madiwani na hata wenye viti wa serikali za mitaa.Tumetambua umuhimu wa
mlango huo wa siasa na ndio maana leo tumekutana na viongozi kutoka
Baraza la Vyama vya Siasa nchini na Msajili ili tujadiliane kwa pamoja
na kuweka malengo ya kutupeleka mbele".
Amesisitiza
ni kweli wanaweza kufurahia kuwa na Rais mwanamke pamoja na Spika wa
Bunge mwanamke lakini hiyo haina maana sasa wakarudi nyuma katika
jitihada ambazo wamekuwa nazo."Huu si wakati wa kubweta na kurudi nyuma,
huu ni wakati wa kuendelea kuweka mikakati zaidi ili kupata wanawake
wengi zaidi katika nafasi za uongozi."
Kwa
upande wake Mkurgenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Lilian
Lihundi amesema pamoja na mambo mengine wamefanya uchambuzi wa Katiba na
Ilani za vyama vya siasa ambapo wamebaini bado kuna ushiriki mdogo
wanawake ingawa kumekuwepo na majukwaa ya wanawake.
"Tunachotaka
wanawake na wanaume washiriki kikamilifu katika masuala yanayohusu
maamuzi na uongozi na hapo ndipo tutakuwa na maendeleo jumuishi na
endelevu nchini kwetu.Kwa mfano wakati wa kuchambua Katiba na Ilani za
vyama vya siasa tumegundua miundo ya kutoa maamuzi kwenye vyama haitoi
nafasi ya kutosha kwa wanawake,"amesema Lihundi.
Awali
wakati akifungua mkutano huo, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Mohamed
Ali Ahmed amepongeza kwa wadau hao kwa kuchagua njia ya majadiliano
katika kuzungumzia usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi."Leo
mngekaa wanawake peke yenu tungesema mnatuteta, tungesema mnajambo
ambalo si nzuri dhidi yetu, lakini mmeamua kutushirikisha wanaume.
"Hali
hii tunayokwenda nayo ya kushirikisha tutafikia malengo ya matakwa ya
katiba zetu, sheria zetu , kanuni zetu pamoja na miongozo ya kimatafaifa
ya kuweka sawa usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume katika
kuongoza nafasi zozote hapa duniani,"amesema.
Ameongeza
harakati za kumpigia mwanamke zimeanza muda mrefu na kuna wakati
wamekwenda mpaka kwenye mkutano wa Beijingi, wamekuwa wakiandaa mijadala
na makongamano."Huko nyuma tulikuwa tunaona jambo la ajabu lakini kumbe
inawezekana , na jitihada hizi haziendi bure hata Mwenyezi Mungu
anazitilia nguvu na ndio maana leo Tanzania ina Rais mwanamke.
Wadau
wa harakati za masuala ya wanawake pamoja na viongozi wa vyama vya
siasa nchini wakiwa katika mkutano uliowakutana kwa lengo la kujadiliana
na kuangalia njia zinazotakiwa kuendelea kufanyika ili kufikia 50 kwa
50 katika nafasi ya uongozi nchini.
"Na
kama alivyosema mwenyewe Rais Samia Suluhu Hassan kuwa amefika pale kwa
kudra za Mwenyezi Mungu , wanaume hatuwezi kujisifia kwa asilimia 100
tumemfikisha pale, bali amefika pale kwa kudra za Mungu, tulichofanya
tulimfikisha kwenye Makamu wa Rais maana tulisema kwa sasa anatosha
mwanamke kufikia makamu wa Rais lakini Mungu akasema hapana ndio maana
tuna Rais mwanamke,"amesema.
Amefafanua
na Tanzania si tu imepata Rais mwanamke , bali imempata mwanamke
anayejua changamoto za wanawake wengine."Tunaweza kuwa na viongozi
wanawake lakini hawawajui wanawake wenzao ni nani.Rais Samia ameanzia
kuwa karani wa masjala hadi kuwa Rais, hivyo anajua changamoto
anazopitia mwanamke ni mwanamke.Kwa hiyo tuseme Mungu analipenda taifa
hili na anawapenda wanawake."
Aidha
amesema ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea kushirikiana na
wadau mbalimbali wakiwemo wa vyama vya siasa kuhakikisha kuna kuwa na
mazingira rafiki ya kumuwezesha mwanamke kushiriki kikamilifu katika
medani za siasa na uongozi.