Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Angeline Mabula amesema wizara yake itaanza ukaguzi na
kuyatambua maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji nchini.
Dkt
Mabula alisema hayo leo tarehe 9 Februari jijini Dodoma wakati
akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka
kuapishwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
‘’Maeneo haya lazima tuyafanyie ukaguzi pamoja na
kuyatambua hasa yale ya vijijini ambayo ardhi yake inahitaji uhaulishaji
ili kupunguza muda wa mwekezaji kusubiri pale anapohitahitaji ardhi ya
kufanya uwekezaji’’ alisema Dkt Mabula
‘‘Vipaumbele vya Wizara
haviwezi kwenda tofauti na vipaumbele vya Rais ambapo Mhe. Rais
ameelekeza suala zima la uwekezaji ambapo sisi kama Wizara tutafanya
ukaguzi wa maeneo yote yaliyotengwa tuyatambue na tujue wenzetu wa TIC,
TAMISEMI, EPZA ardhi walionayo ni kiasi gani na wamepanga kufanya nini’’
alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Halmashauri
kwa maana ya TAMISEMI kupitia mipango kabambe katika maeneo yao kuna
maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na wizara itataka kujua kiasi
gani cha maeneo yaliyopo yamepangwa kwa kwa makusudio gani.
Dkt
Mabula ambaye amechukua kijiti cha uwaziri kutoka kwa William Lukuvi
alisema, jukumu la Wizara ya ardhi litakuwa ni kutwaa maeneo hayo ili
yawe chini yha serikali ili muwekezaji atakapofika serikali itajua
sehemu sahihi kumpeleka kwa kuwa kutakuwa na kanzidata ya maeneo husika.
‘‘Kwenye
maeneo ya Vijiji kuna maeneo mengi ambayo yana fursa nzuri za uwekezaji
ambapo ardhi ya vijiji inasimamiwa na Sheria Na. 5 ili iweze kumilikiwa
inabidi zoezi la uhaulishaji katika maeneo yaliyokusudiwa kuwa ya
uwekezaji lifanyike kwa ukamilifu na kuwe na umiliki wa eneo ili
mwekezaji atakapokuja tusianze kufanya mikutano ya wananchi ili
wakubali’’ alisema Dkt Mabula .
Akigeukia suala la migogoro ya
Ardhi, Dkt Mabula alieleza kuwa migogoro ya ardhi inagusa Wizara tano za
Kisekta na inatokea kwa sababu hapajaweza kuwekewa mpango wa matumizi
ya ardhi kwa nchi nzima na kubainisha kuwa, wizara itazungumza na Ofisi
ya Rais TAMISEMI kwa maana ya halmashauri zote ili kuweza kuona kwa
jinsi gani patakuwa na zoezi la maksudi kabisa la kuhakikisha kwamba
walau vijiji na maeneo mengi yanapangiwa matumizi ya ardhi.
‘‘Bila
kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi migogoro haiwezi kuisha na
tukipanga na kuheshishimu makubaliano yaliyowekwa katika maeneo hayo ni
wazi migogoro itapungua, ili kufanikisha hili inahitaji ushirikiano wa
Wizara Tano za Kisekta’’ alisema Dkt Mabula.
Kwa upande wa zoezi
la anuani za makazi, Waziri wa Ardhi alisema kipaumbele cha Wizara yake
itakuwa kwenda kwa kasi kubwa katika suala zima la upimaji maeneo
pamoja na kutambua wamiliki wa maeneo hayo. ‘’Kwetu sisi Wizara katika
zoezi la anwani za makazi limepewa kipaumbele kikubwa kwamba tukizembea
tutakuwa tumekwamisha zoezi zima’’ alisema Dkt Mabula.