Ikulu ya Marekani Jumatano imeshinikiza Iran waziwazi kwamba ifufue kwa haraka mkataba wa nyuklia wa 2015, ikiongeza kwamba itakuwa vigumu kwa hilo kufanyika, wiki chache kuanzia sasa.
Msemaji wa ikulu Jen Psaki wakati akizungumza na wanahabari ,alisema kwamba mazungumzo yao na Iran yamefikia hatua ya dharura na kwamba mjumbe maalum wa Marekani nchini Iran, Rob Malley amerudi mjini Vienna ili kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Iran, kuhusu pande zote mbili kurejea kwenye mkataba huo.
Psaki amesema kwamba mkataba unaozingatia maslahi ya pande zote mbili umekaribia, lakini iwapo hautafikiwa ndani ya wiki kadhaa zijazo, basi itakuwa vigumu kurejea kwenye mkataba huo maarufu kama JCPOA, kutokana na hatua za kinyuklia zilizopigwa na Iran kufikia sasa.
Matamshi ya Psaki yanafuatia yale ya afisa wa ngazi ya juu kwenye wizara ya mambo ya nje ya Marekani, ambaye Januari 31 alisema kwamba kuna muda wa wiki kadhaa uliobaki wa kufufua mkataba huo. Mkataba huo ulilenga kudhibiti program ya nyuklia ya Iran dhidi ya utengenezaji wa silaha hatari za nyuklia.