HIVI karibuni serikali ilitoa takwimu zikionesha utumikishwaji wa watoto umepungua kutoka asilimia 29 mwaka 2014 hadi asilimia 24.9 mwaka 2021.
Hata hivyo, ilisema licha ya takwimu kuonesha kupungua huko kwa utumikishaji watoto nchini, changamoto ya ajira kwa watoto bado ipo kwenye sekta za kilimo, migodi, kazi za nyumbani na ajira zisizo rasmi mijini.
Akizungumza jijini Dodoma katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Watoto, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alisema watoto wengi hujikuta wakitumikishwa kwa masilahi ya kiuchumi ya familia zao au waajiri.
Kutokana na kuendelea kwa tatizo hilo, alisema serikali imepanga kufanya ukaguzi maalumu kwa wiki mbili na kuendelea, awamu kwa awamu kwenye maeneo mbalimbali kuwabaini na kuwachukulia hatua wanaotumikisha watoto.
Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2019 pamoja na mambo mengine inakataza utumikishwaji wa watoto kwani unawanyima haki za msingi ikiwamo elimu, afya na kushiriki katika masuala ya rika lao.
Tunaunga mkono hatua hiyo ya serikali kuwasaka waajiri wanaotumikisha watoto katika kazi zisizo na staha na nje ya uwezo wao wa kiakili na kimwili na kuishauri serikali isiwafumbie macho hata kidogo.
Tunaamini hatua kali zikichukuliwa, itakuwa fundisho kwa wengine na litajengwa taifa lenye kuheshimu hali za binadamu wakiwemo watoto ambao wanastahili kuwa shule lakini wanatumikishwa isivyo stahili.
Tunaamini pamoja na wiki mbili kumalizika, bado kutakuwa na kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na huru dhidi ya ajira haramu.
Pamoja na maeneo mengine, tunashauri timu za ukaguzi zijikite katika maeneo ya migodi, mashamba, viwanda na makazi ya watu, yaani nyumba kwa nyumba ili kwa walioajiri wafanyakazi wa ndani wanaopaswa kuwa shule hasa elimu ya msingi, wachukuliwe hatua.
Tunafahamu kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulamavu kwa kushirikiana na wadau imeanzisha Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Watoto ambao unalenga kuunganisha nguvu za wadau wote wa maendeleo, mashirika ya kiraia na jamii kwa ujumla.
Tunafahamu ukaguzi huu unaoendelea ni sehemu ya mkakati huo. Hivyo, tunashauri matokeo ya ukaguzi yawekwe bayana kwa jamii ili watu wasiopenda kutii sheria bila shuruti, wajue watafikiwa na mkono wa sheria na kuchukuliwa hatua kali.
Katika siku hiyo ya kupinga utumikishwaji wa watoto kimataifa, Mratibu wa Miradi Kitaifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Glory Blasio aliipongeza Tanzania kwa hatua kubwa ya kukabiliana na utumikishaji huo huku akisema kwa kiasi kikubwa utumikishaji bado upo kwa watoto wa kike.
Pongezi hizi tunashauri ziwe chachu ya kuongeza kasi kutokomeza tatizo hilo. Kwa pamoja tunaweza kuwaweka watoto wa Kitanzania huru dhidi ya utumikishwaji haramu.