Msajili wa Vyama Vya Siasa hana mamlaka ya Kuzuia Chadema kushiriki uchaguzi mkuu

Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kukizuia Chama hicho kushiriki shughuli za siasa kwenye mwaka wa uchaguzi.

Mbali na hilo pia Lissu ameiomba mahakama hiyo kuwa kama upelelezi ama ushahidi haujakamilika basi aachiwe huru kwa sababu mara ya mwisho waliambiwa upelelezi umekamilika na jalada lipo wa DPP.

Lissu ameyasema hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Franko Kiswaga wakati lilipotajwa shauri la uhaini ambapo ilitarajiwa upande wa Jamhuri kutoa taarifa juu ya uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kama kesi hiyo iende Mahakama Kuu ama lah.

Lissu alisema kuwa anaiomba mahakama hiyo isiahirishe kesi kwa sababu hakuna sababu ya msingi, kwani mara ya mwisho waliambiwa upelelezi umekamilika na wangepewa taarifa ya uamuzi.

Akiwa kizimbani Lissu alihoji kwamba inamchukua muda gani DPP kusoma faili la kesi hiyo hali ya kuwa yeye ni msomi wa sheria na kama upelelezi ama ushahidi haujakamilika basi aachiwe.

“Kwa mujibu wa Katiba, Msajili hana mamlaka hata kama ana sababu ya kutuzuia kushiriki uchaguzi Mkuu, kama hakuna ushahidi basi niachiwe,”

Kwa upande wa Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga alisema kuwa kutokana na shauri hilo kuwa na maslahi kwa umma ndio maana wameomba ahirisho ili waje kusema kwamba jalada limefikia hatua gani.Pia DPP amefanya jitihada za kutosha kuhusu hiyo licha ya kuwa na majukumu mengi.

Kutokana na mvutano huo kwa kisheria, Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 15, 2025. 

“Kabla sijanyanyuka, nitoe maelekezo kwa wahusika wa shauri hili, Maafisa wa Mahakama na wote ninatambua kuwa shauri hili lina mvuto na lina vutia watu wengi lakini inatakiwa kufuata sheria,  ukifika tulia kaa kuna vitu vinaendelea kabla shauri halijaendelea ama mahakama kuanza mtu anaibuka anafanya vitu visivyofaa ni marufuku kufanya chochote kile, Maafisa wa Mahakama, Mawakili wa Seikali na Kujitegemea nafikiri mfahamu hilo”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii