Félix Tshisekedi arejelea makubaliano ya amani katika hotuba yake kwa taifa

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeadhimisha miaka 65 ya uhuru siku ya Jumatatu, Juni 30. Wakati wa hotuba yake kwa taifa, Mkuu wa Nchi Félix Tshisekedi amezungumza kwa kirefu kuhusu mkataba wa amani uliotiwa saini kati ya nchi yake na Rwanda siku ya Ijumaa, Juni 27, mjini Washington. Anachukulia hii kuwa hatua muhimu ya kumaliza mzozo ambao umesababisha uharibifu katika eneo la mashariki mwa nchi kwa karibu miongo mitatu.

"Makubaliano haya ya amani yanafungua njia kwa enzi mpya ya utulivu," rais Tshisekedi amesema wakati wa hotuba yake. Hata hivyo, "amani hii muhimu inaendelea kuwa tete," ameonya, akiongeza kwamba "Sote tunahitajika kujitolea kwa dhati kwa mpango huu." 

Kuhusu suala nyeti la fidia kwa uhalifu uliotendwa mashariki mwa nchi hiyo—ambalo halimo katika makubaliano ya amani ya Washington—ameahidi kuendelea kudai haki kwa wahasiriwa na kwamba waliohusika na ukatili huo wawajibishwe.

Suala jingine nyeti ni uuzaji wa madini nchini Marekani. Mkuu wa Nchi amethibitisha kusainiwa kwa makubaliano na Wamarekani siku zijazo katika sekta ya madini, zoezi ambalo litafanyika DRC "mshiriki mkuu katika mpito wa nishati duniani," amehakikisha, kabla ya kuongeza kuwa manufaa ya kiuchumi yatanufaisha watu wa Kongo na kuahidi kuwa rasilimali za nchi hazitauzwa kamwe na kwamba hakuna maelewano yatakayozigatiwa.

Hatimaye, Mkuu wa Nchi alizungumzia suala la umoja wa kitaifa. "Ni wakati wa kuipa kisogo migawanyiko." "Ni katika hali hii kwamba nilikutana na Martin Fayulu," amesema, akielezea mazungumzo yake na kiongozi wa upinzani kama hatua muhimu kuelekea sera ya maridhiano.

Rasilimali za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hazitawahi kuuzwa au kukabidhiwa kwa maslahi ya siri. Zitanufaisha, mbele ya yote, raia wa Kongo. Hakuna maelewano yatakayovumiliwa katika masuala ya uhuru wa kiuchumi.

Wito wa "mazungumzo jumuishi ya kitaifa"

Martin Fayulu pia amesema siku ya Jumatatu, Juni 30, kwa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mjini Washington. Wakati wa hotuba yake ya kuadhimisha miaka 65 ya uhuru wa DRC, alitoa picha mbaya ya hali ya usalama na uchumi wa nchi hiyo.

"Makubaliano haya, ingawa hayawezi kubatilishwa, yanaweza kuwakilisha fursa ya kurejesha utulivu," ameongeza mpinzani huyo, ambaye anatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutekeleza maazimio ya kulaani mashambulizi ya waasi wa M23 na ambaye anatoa wito juu ya yote "mazungumzo jumuishi ya kitaifa bila kuchelewa, kwa sababu wakati sio tena wa uadui usio na msingi bali wa maridhiano na mshikamano wa kitaifa."


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii