Kuzindua upya msaada wa kimataifa kwa maendeleo

Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo umefunguliwa siku ya Jumatatu hii, Juni 30, huko Seville, nchini Uhispania, huku kukiwa na upungufu mkubwa wa misaada ya maendeleo, hasa kutokana na kuvunjwa kwa shirika la Marekani la Misaada ya Kimataifa (USAID).

Takriban wakuu 70 wa nchi na serikali wanatarajiwa kukusanyika mjini Seville kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi kwa ajili ya mkutano huu unaoitwa "FfD4", pamoja na wawakilishi 4,000 kutoka mashirika ya kiraia na taasisi kuu za kifedha za kimataifa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatumai mkutano huu utasaidia kupata "suluhu" kwa mahitaji makubwa ya nchi zinazoendelea, ambazo "zinakabiliwa na pengo la kila mwaka la ufadhili la dola Trilioni 4," sawa na dola Trilioni 1.5 zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Mbali na Antonio Guterres na Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, na Mkuu wa Benki ya Dunia Ajay Banga pia wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo. "Tunakabiliwa na changamoto kubwa leo," amebainisha Pedro Sanchez, akikumbusha kwamba matatizo haya ya ufadhili yalikuwa yanadhoofisha ushirikiano wa pande nyingi, pamoja na "malengo ya maendeleo endelevu" na mapambano dhidi ya "mgogoro wa tabianchi."

"Katika mazingira haya yenye msukosuko, hatuwezi kuruhusu matarajio yetu kufifia," ameonya Antonio Guterres, ambaye anaona mkutano huu kama "fursa ya kipekee ya kurekebisha mfumo wa fedha wa kimataifa," unaochukuliwa kuwa "wa kizamani" na "usiofanya kazi." Rasimu ya tamko iliyopitishwa kabla ya mkutano inaunga mkono hili, ikisisitiza kwamba mfumo wa kifedha lazima uendane na "hali halisi ya ulimwengu unaobadilika," haswa kwa kutoa nafasi kubwa kwa nchi za Kusini mwa Ulimwengu ndani ya taasisi za kifedha za kimataifa. Kwa hivyo benki za maendeleo zimetakiwa "kuongeza mara tatu" uwezo wao wa kukopesha, wafadhili "kuhakikisha ufadhili unaotabirika" kwa matumizi muhimu ya kijamii, na jumuiya ya kimataifa kuboresha "ushirikiano" katika kukabiliana na ukwepaji wa kodi.

Hata hivyo, hakutakuwa na mwakilishi wa Marekani katika mkutano huu mkuu huko Seville. Hili ni jambo la kimantiki, kufuatia kupunguzwa kwa ufadhili wa 83% kwa programu za ng'ambo na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) hatua iliyochukuliwa na Donald Trump mwanzoni mwa mwaka.

"Ni muhimu sana kuwa wazi"

Kabla ya mkutano huu wa Seville, mkutano wa ngazi ya juu ulifanyika siku ya Ijumaa, Juni 27 huko Paris, katika Chuo Kikuu cha Ufaransa, ambao uliandaliwa na hirika la J-Pal la mshindi wa Tuzo ya Nobel katika uchumi, Esther Dufflo. J-Pal, mtandao wa watafiti wa uchumi na wataalamu wa maendeleo, unafanya kazi ya kupunguza umaskini. "Kupunguza umaskini kwa kiasi fulani kutahusisha sekta ya kibinafsi, kwa sababu ni muundaji mkuu wa utajiri," anaelezea Dean Karlan, profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Northwestern na mwanauchumi mkuu wa zamani wa USAID.

"Kuna nyanja nyingi ambazo sekta binafsi ni, kwa kweli, chombo bora kwa mabadiliko ya kijamii. Wakati kampuni ya sekta binafsi ina athari kubwa ya kijamii, hiyo ni nzuri. Na hiyo ndiyo suluhisho bora zaidi. Na kisha, katika mtazamo wangu wa ulimwengu, wakati sivyo, basi ni juu ya serikali kuchukua hatua ili kuchangia manufaa ya umma, " anaeleza Dean Karlan.

Abhijit Banerjee ni mchumi wa maendeleo na mpokeaji mwenza wa Tuzo ya Nobel ya Uchumi. Kwake, suala la kufuta sehemu ya deni la nchi zinazoendelea ni muhimu. Suala lingine muhimu: hitaji la uwazi zaidi.

"Jambo la kwanza ni kwa urahisi, nadhani, nia ya kutofautisha kati ya mikopo na misaada. Kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusu mikopo, uwekezaji wa sekta binafsi, na kadhalika. Hebu angalau tuwe wazi juu ya nini ni misaada ya kweli. Mikopo mingine inaweza kuwa msaada, lakini tunahitaji kuwa na uwezo wa kutathmini kwa thamani yake halisi. Vinginevyo, hakuna mtu anayelazimika kusema ukweli ikiwa ni muhimu sana. Kwa hivyo nadhani ni nani anayeweza kuamua wazi zaidi. nini kwa nani na kwa nini, na ni vipaumbele gani jumuiya ya kimataifa iko tayari kukubali kwa kweli na kwa uaminifu, itakuwa na mafanikio," anasema Abhijit Banerjee, ambaye anaangazia, kwa mfano, hitaji la mifumo iliyo wazi yenye vigezo vinavyoweza kufikiwa vya ufadhili wa tabianchi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii