CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepiga marufuku kwa mwanachama yeyote anayeomba kugombea uongozi kualika kundi la wapambe kumsindikiza kwenda ofisi za chama kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea.
Pia, kimepiga marufuku kwa mwanachama kuandaa msafara wa magari, pikipiki, baiskeli, ngoma na matarumbeta ya kumsindikiza kwenda ofisi za CCM kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea.
Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Oganaizesheni, Issa Ussi Gavu amesema hatua hiyo inatokana na mwongozo na maelekezo kuhusu utaratibu wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wanachama wa CCM wanaoomba kugombea uongozi katika vyombo vya dola 2025.
Alisema mchakato wa ndani wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea uongozi katika vyombo vya dola utaanza Juni, 28 mwaka huu.
Ussi alisema ili kusimama na kulinda misingi ya chama katika kuwaunganisha wanachama wake, chama hakina budi kuimarisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano.
“CCM inakumbusha viongozi, watendaji na wanachama kuendelea kufuata maadili ya uchaguzi kama ilivyoainishwa kwenye katiba, kanuni za uchaguzi wa CCM na miongozo yake,” alieleza Ussi.
Mwaka 2020, chama hicho pia kilipiga marufuku wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi kutumia matarumbeta wakati wa kwenda kuchukua fomu za kugombea, badala yake waende kimya kimya na matarumbeta yatapigwa baada ya chama kumteua mgombea.
Katika mkutano maalumu wa CCM uliofanyika Mei 30, mwaka huu jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan alisema mchujo wa wagombea ni wa lazima na utafanyika kwa haki, uadilifu na kwa kuzingatia maslahi ya
chama na taifa kwa ujumla.
Alisema si kila mtu anayejitokeza kuwania nafasi za uongozi anastahili kupitishwa, hivyo ni wajibu wa vikao husika kuwachuja wagombea kwa misingi ya sifa, uwezo na maadili, badala ya kufuata ushawishi wa muda mfupi au makundi ya maslahi.
“Vikao vinavyokwenda kuchuja wagombea vikatende haki. Anayefaa aambiwe anafaa. Asiyefaa, tuseme wazi kuwa ana kasoro na hatufai huko tunapokwenda,” alieleza.
Alisisitiza kwamba CCM haitaki kuwa chama cha watu wanaotafuta madaraka bila maono wala maadili ya kiuongozi na kwamba kuwapitisha wagombea wasiostahili ni kuhatarisha mustakabali wa chama.