Iran yatoa tahadhari nchini Marekani kuhusu mashambulio

 KIONGOZI Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesema taifa lake liko tayari kujibu kwa nguvu kubwa endapo Marekani itafanya shambulio lolote dhidi ya Iran, akibainisha kuwa majeshi ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati yako katika hatari.

Akihutubia kwa mara ya kwanza tangu kusitishwa kwa mapigano kati ya Iran na Israel, Khamenei alisema mashambulio yoyote dhidi ya Iran yatakabiliwa kwa gharama kubwa kwa upande wa Marekani.

Hata   hivyo kuna uwezo wa kujibu shambulio lolote litakalofanywa na adui kwa kulenga kambi za kijeshi za Marekani zilizopo katika Mashariki ya Kati.

Viongozi hao wawili wametoa kauli zenye kuashiria kuendelea kwa mvutano wa kijeshi na kisiasa, hasa kutokana na tofauti zao kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Khamenei pia alimshutumu Rais wa Marekani wa wakati huo, Donald Trump, kwa kile alichokieleza kuwa ni kutia chumvi kuhusu madhara ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.

Alisema kuwa mashambulizi hayo  hayakuathiri kwa kiwango kikubwa uwezo wa Iran wa kuendeleza mpango wake wa nyuklia.

Awali Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth, alikanusha ripoti za kiintelijensia zilizodai kuwa mashambulizi ya Marekani yalisababisha ucheleweshaji wa miezi mitatu tu katika maendeleo ya nyuklia ya Iran, bila kuharibu kabisa miundombinu ya mradi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Trump alinukuliwa akisema kuwa iwapo Iran itajaribu kuanzisha tena mpango wake wa nyuklia hakika Marekani itajibu kwa nguvu.

Mvutano huo unaendelea huku jumuiya ya kimataifa ikihimiza pande hizo mbili kurejea katika meza ya mazungumzo ili kuepusha kuibuka kwa mzozo mpya wa kijeshi katika eneo hilo tete.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii