Tuzo za Utalii Duniani (WTA) kwa Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi mwaka 2025 zitafanyika Jumamosi, Juni 28, 2025 jijini Dar es Salaam huku Tanzania ikiwania vipengele 50.
Akizungumza leo Alhamisi, Juni 26, 2025 jijini Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana amesema tukio hilo linaonesha hadhi kubwa ambayo nchi imejipatia kimataifa katika sekta ya utalii.
Dk Chana amesema Tanzania itashiriki katika vipengele 50 vya tuzo hizo ikiwa ni pamoja na Eneo Bora la Utalii Afrika, Kivutio Bora cha Utalii, Bodi Bora ya Utalii, Hifadhi Bora Afrika, Hoteli Bora kwa Watalii na Kampuni Bora za Safari.
Amesema ushiriki huo ni matokeo ya jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya The Royal Tour na Amazing Tanzania.
Amesema zaidi ya washiriki 250 kutoka nchi mbalimbali tayari wamethibitisha kushiriki wakiwemo viongozi wa sekta ya utalii, wawekezaji, waandishi wa habari wa kimataifa na watoa huduma wa sekta hiyo kutoka Afrika na visiwa vya Bahari ya Hindi.
Dk Chana ametoa wito kwa Watanzania kujivunia nafasi hiyo ya kihistoria na kumshukuru Rais Samia kwa kuendeleza sera, miundombinu na uwekezaji unaoifanya Tanzania kuendelea kung’ara kimataifa kama kitovu cha utalii Afrika.
Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 1993 nchini Uingereza na zimekuwa zikitolewa kwa mfululizo kwa miaka 32, zikilenga kutambua ubora katika huduma za utalii duniani.
Tanzania ilianza kushiriki mwaka 2013 na imekuwa ikijizolea tuzo kila mwaka, ikiwemo ile ya Kivutio Bora kupitia Mlima Kilimanjaro.