Kumalizika kwa tundu jipya la reli mita 602 launganisha China na Urusi

SERIKALI ya China imekamilisha ujenzi wa tundu jipya la reli lenye urefu wa mita 602 katika mji wa Suifenhe, Heilongjiang, hatua inayolenga kuimarisha usafiri wa reli kati ya China na Urusi.

Ujenzi wa tundu hilo ulianza Mei mwaka jana na sasa limeunganisha Suifenhe na mpaka wa Urusi, kupitia njia ya reli itakayowezesha treni kusafiri kwa kasi ya hadi kilomita 120 kwa saa.

Miundombinu hiyo mipya inatarajiwa kuongeza uwezo wa njia hiyo katika kusafirisha abiria na mizigo kwa ufanisi zaidi. Suifenhe ni kitovu muhimu cha kibiashara kati ya China na Urusi, na kukamilika kwa tundu hilo kunatarajiwa kurahisisha na kuharakisha shughuli za usafiri na biashara.

Tundu hilo limejengwa kwa kutumia teknolojia za kisasa na linakidhi viwango vya kimataifa vya reli za kasi kubwa.Mradi huu unakuja wakati ambapo ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Urusi unaendelea kuimarika.

Maboresho hayo ya reli yanalenga kuongeza wingi wa biashara kwa kuharakisha usafirishaji wa bidhaa, rasilimali na mazao ya kilimo kati ya mataifa hayo jirani.

Aidha, tundu hilo ni sehemu ya juhudi za China kupitia mpango wake wa kupanua sekta ya usafirishaji unaotambulika kama (Belt and Road Initiative), unaolenga kuunganisha nchi jirani kupitia miundombinu ya kisasa.

Kukamilika kwa mradi huo kunaweka msingi thabiti wa ukuaji wa muda mrefu wa biashara katika mpaka wa China na Urusi. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii