Milionea kutoka Jamhuri ya Czech Radim Passer anakumbwa na uchunguzi wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa Ujerumani.
Mmiliki huyo wa gari aina ya Bugatti Chiron alichapisha video ya jinsi alivyoongeza kasi hadi 417 km / h kwenye gari lake kwenye barabara moja katika eneo la Saxony-Anhalt huko Ujerumani msimu uliopita wa joto .
Hakuna kikomo rasmi cha kasi kwa magari ya Ujerumani, lakini ikiwa ofisi ya mwendesha mashitaka wa jiji la Stendal atapata uhalifu katika vitendo vyake, anaweza kufungwa jela miaka miwili, au angalau faini kubwa.
Hali hiyo imezidishwa kuwa mbaya baada ya kugundulika kwamba mnamo 2015 Passer tayari alikuwa akiongeza kasi kwenye barabara moja ya nchi hiyo hadi 400 km / h katika Bugatti Veyron.
Mara zote mbili alichapisha video kwenye YouTube, na zimetazamwa zaidi ya mara milioni 10.
Waziri wa Uchukuzi wa Ujerumani Volker Wissing alilaani tabia ya dereva huyo akibainisha kuwa ingawa hakuna vizuizi vya mwendo kasi kwenye barabara za magari, gari lazima liwe na udhibiti kila wakati.