Samia ataka amani, umoja wa Afrika kufanikisha mageuzi ya kifikra

RAIS Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi za Afrika kuhakikisha zinakuwa na amani na umoja wa kitaifa ili zishirikiane kufanikisha hatua za mageuzi ya kifikra na kutafuta uhuru wa kiuchumi.

Akizungumza kwenye maadhimisho wa miaka 50 ya uhuru wa Msumbiji mjini Maputo, Rais Samia amesema Afrika imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika hatua ya kwanza ya ukombozi kwa kuwa na uhuru wa kisiasa, hivyo hatua inayofuata ni kutafuta uhuru wa kiuchumi.

Rais Samia alisema katika kufanikisha hilo, hatua mojawapo ni kuhakikisha wanaunganisha watu kwa kuleta umoja wa kitaifa.

Katika sherehe hizi  tumeshuhudia uwepo wa Mwenge wa Uhuru, mwenge ambao umetembezwa nchi nzima kwa nia ya kuwaleta watu pamoja na kuamsha ari ya mshikamano na uzalendo, niwaombe kuendeleza jitihada hizi, kwani kupitia mwenge huu, heshima na matumaini ya wananchi yanakwenda kuamshwa.

Jitihada hizo ziende sambamba na kuhakikisha wananchi wanakuwa na imani na nchi yao, waweze kutanguliza maslahi ya nchi kabla ya kwao wenyewe, kulinda na kuhifadhi rasilimali za nchi kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wananchi.

Alisema katika kufanya hayo, ipo haja ya kumuinua mwanamke kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

“Ni kwa sababu hiyo, ninawapongeza sana kwa kuchagua kaulimbiu ya mbio za Mwenge wa Umoja wa Kitaifa za mwaka huu isemayo ‘Miaka 50: Kuwainua Wanawake, Kujenga Usawa wa Kijinsia’,” alisema.

Rais Samia alisema ni fahari kubwa licha ya mtazamo hasi kuhusu nafasi ya mwanamke kwenye jamii katika miaka ya 1960, wanawake wa Msumbiji walijitolea kuwa mstari wa mbele kwenye mapambano ya uhuru wa nchi yao.

“Hatuna budi kuwatambua wanawake waliochangia harakati za ukombozi ambao wanaingia katika vitabu vya historia… na wanawake wengine wengi, ambao walishiriki sio tu kupigania uhuru wa Msumbiji, bali pia kumuinua mwanamke kutoka aina zote za ukandamizaji,” alisema.

Alisema wanawake hao na wenzao, wanawakumbusha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika ustawi na maendeleo kwa jamii ya wanawake, ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya, maji, elimu na umeme.

“Katika hilo, niwapongeze sana viongozi na wananchi wa Msumbiji kwa hatua kubwa zilizochukuliwa, kama ile ya kuwekeza kwenye miundombinu na huduma za afya zilizochangia kupungua kwa vifo vya wajawazito na watoto wakati wa kujifungua,” alisema.

Aidha, Rais Samia alisema Afrika haina budi kuendelea kuchukua hatua kuwawezesha wanawake na vijana kunufaika zaidi na fursa zitokanazo na utangamano wa kikanda na soko la Afrika kwa ujumla.

“Umoja wa Afrika umepitisha Itifaki ya AfCFTA ya wanawake na vijana kwenye biashara inayolenga kujibu baadhi ya changamoto zinazoyakabili makundi haya na kuyazuia wasifaidike na fursa zinazotengenezwa na soko la kikanda,” alisema.

Aidha, katika kuzidi kufungua fursa zaidi za biashara baina ya wananachi wa Msumbiji na Tanzania, Rais Samia alisema Kampuni ya Ndege la Tanzania (ATCL) inatarajia kuanza safari za ndege kati ya Tanzania na Msumbiji mwisho wa mwaka huu, hatua itakayoimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya watu wa nchi hizo.

“Ninaamini chini ya uongozi mahiri wa Rais Daniel Chapo, watu hodari wa Msumbiji wataendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo, na ninataka nikuahidi kuwa, Tanzania itaendelea kuwa nawe bega kwa bega katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo,” alisema.

Alisema Tanzania na Msumbiji si majirani tu waliotenganishwa na Mto Ruvuma, bali ni ndugu wa damu.

“Udugu wetu uliimarishwa zaidi na waasisi wetu, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Dk Eduardo Mondlane na baadaye Samora Machel wa Msumbiji, kupitia viongozi hao, wananchi wetu walifanya kazi bega kwa bega wakati wa harakati za ukombozi na hatimaye kuweza kupata uhuru wa Msumbiji tunaouadhimisha leo (jana),” alisema.

Tangu uhuru Juni 25, 1975, Msumbiji inaongozwa na Chama cha Frelimo, chama cha uhuru kilichoasisiwa na rais wa kwanza Machel, aliyeongoza tangu uhuru hadi mwaka 1986 alipopoteza maisha kutokana na ajali ya ndege.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii