Wanahabari watakiwa kuhimiza uadilifu kuelekea uchaguzi mkuu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro imewataka waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kupinga na kuzuia vitendo vya rushwa, hasa kipindi hiki cha kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu (2025).

Mkuu wa Takukuru Mkoa huo, Pilly Mwakasege amesema hayo wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari Mkoa wa Morogoro yanayohusu sheria na kanuni za kukabiliana na rushwa hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.

Mwakasege amesema waandishi wa habari wana nafasi pekee ya kuhamasisha jamii kuchukia rushwa na kutoishiriki katika maeneo yote ya maisha yao, ikiwa ni pamoja na kwenye mchakato wa kupata viongozi wa kisiasa.

Hata hivyo amewasihi wanahabari kuhakikisha wanafichua na kuripoti vitendo vyote vya rushwa ambavyo vinafanyika siri au hadharani katika mikutano ya kisiasa, ugawaji wa vyeo au maeneo mengine yanayohusiana na uchaguzi.

Mwakasege amesema rushwa huchangia uchaguzi usio huru na wa haki, na hivyo ni lazima waandishi wa habari watumie vipindi vyao, makala na taarifa mbalimbali kuelimisha wananchi juu ya haki yao ya msingi ya kugombea na kuchagua viongozi wanaowataka bila kununuliwa kwa rushwa.

“Mafunzo haya  ni sehemu ya mpango kazi wa Takukuru kuwashirikisha wadau wote katika mapambano ya rushwa, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari ambavyo vinabebwa kama dira ya jamii,” amesema Mwakasege.

Naye mtoa mada katika mafunzo hayo ambaye ni Ofisa wa Takukuru , Herry Mwankusye amesema kuwa uelewa wa wananchi kuhusu rushwa na vita dhidi yake umekuwa ukiongezeka na hivyo kuwapa hamasa kushiriki zaidi katika mapambano dhidi ya rushwa.

Pia amesema nidhamu kwa watumishi wa umma imeendele kuongezeka kwa kuwatumikia vizuri wananchi badala ya kujali maslahi yao binafsi.

Mwankusye amesema kuwa huo ni uthibitisho kuwa rushwa unapungua nchini na kwamba maoni ya wananchi kupitia tafiti mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinaonyesha kuwa Rushwa unapungua nchini.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa huo, Christopher Mwakajinga akihitimisha mafunzo hayo amesema kuwa waandishi wa habari ni sauti kwa wasio na sauti kwenye jamii .

Mwakajinga amewashauri waandishi wa habari kuangalia zaidi changamoto zilizopo kwenye maeneo yao badala ya zile za kitaifa kuzipa kipaumbele hususani maeneo wanayosimamia  madiwani badala ya kuwadharau kwani wao ndio wasimamizi wa miradi ya maendeleo kata zao na halmashauri kwa ujumla wake.

“Madiwani ndio wanaunda Baraza la Madiwani la Halmashauri, unaweza kusema ndilo bunge linalipitisha shughuli za maendeleo ya halmashauri, hivyo wananchi wanayo hali na kupata taarifa sahihi,” amesema Mwakajinga.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii