MAMLAKA ya Mapato (TRA) mkoani Kigoma imeteketeza bidhaa mbalimbali za vyakula na vipodozi tani 53 zenye thamani ya Sh milioni 530 ambazo ziliingizwa nchini bila kufuata taratibu.
Meneja wa TRA mkoani humo, Beatus Nchota ametoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari wakati wa uteketezaji wa bidhaa hizo katika dampo la kuputia uchafu lililopo Buhanda Businde Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma.
Kiongozi huyo amesema bidhaa hizo ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu zilikamatwa kwa kipindi cha miaka miwili katika operesheni mbalimbali zilizofanywa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama zikiwa hazina vibali vya mamlaka.
Bidhaa zilizokamatwa zimetajwa kuwa ni pamoja na vipodozi haramu aina ya Pawpaw Cream, Cocopulp, Epidem, vinywaji vya kusisimua mwili vikiwemo akayabagu na eloko ya mibali, pombe kali aina ya warag, amstel, pendo gin, hozagara na akanovera, sigara hatari aina ya bharat na super mathc zikiwemo pia nyavu zilizopigwa marufuku, dawa za binadamu na sikari.
Meneja wa Kanda ya Magharibi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA), Christopher Lugoa amesema kuwa ameshiriki kwenye utekelezaji wa shehena hiyo kutokana na mamlaka za kisheria kuipa TMDA mamlaka ya kuthibitisha kwamba bidhaa za vyakula na dawa vilivyokamatwa kwa wakati huo hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Naye ofisa udhibiti ubora wa bidhaa wa Shirika la Viwango (TBS) Kanda ya Magharibi, Ezekiel Mobuti amesema kuwa sheria imewapa mamlaka ya kusimamia viwango mbalimbali vya kitaifa na kimataifa vilivyowekwa na kwamba bidhaa ambazo hazijafikia viwango vinapaswa kutekekezwa kama ambavyo katika bidhaa zilizokamatwa zipo ambazo hazijapata vibali vya TBS kwa ajili ya kutumika nchini.