Mwanza wanufaika na utekelezaji mpango wa fedha za TASAF

 MKOA wa Mwanza umetumia zaidi ya Sh bilioni 50.3 ambazo zimelipwa kuanzia mwaka 2014 hadi mwezi Juni mwaka huu kama ruzuku kwa kaya kwaajili ya  wanufaika wa mpango huo awamu ya tatu kipindi cha kwanza mkoani humo.

Hayo yamesemwa Juni 25 mwaka huu jijini Mwanza na Mratibu wa TASAF, Mkoa  Monica Mahundi alipotoa taarifa ya utekelezaji wa mpango huo kwa umoja wa wanawake wenza na viongozi ambao wako mkoani Mwanza kwa ziara ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF.

Amesema kwa  upande wa  TASAF III kipindi cha pili yalifanyika malipo ya fedha za ruzuku kwa awamu 17 ambapo kiasi cha Sh bilioni 47.6 kililipwa kwa kaya nufaika 51,045.

Ameeleza kuwa kati ya kaya hizo, kaya 29,264 zilipokea fedha zao za ruzuku kupitia benki na mitandao ya simu ambapo kiasi cha Sh bilioni 36.5  kililipwa kwa kaya 21,78 na kupokea fedha taslimu kiasi cha Sh bilioni 11.12.

Ameenelea kufafanua kuwa utambuzi wa kaya maskini kwa kipindi cha kwanza na cha pili ulihusisha jumla ya mitaa yote 346 na jumla ya vijiji 544 vya Mkoa wa Mwanza ambapo jumla ya kaya 100,387 zilitambuliwa na kupitishwa katika mfumo wa uhakiki wa kompyuta kwa kutumia vigezo vya utambuzi vilivyowekwa. 

Aidha amesema mpango huo pia umeziwezesha kaya maskini kujiongezea kipato kwa kutoa ajira za muda kwa mwaka, kwa kaya zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi ambao hupewa ajira na kufanya kazi kwenye miradi iliyoibuliwa katika jamii na kujiongezea kipato.

Awali akizungumza na wajumbe wa wanawake  wenza na viongozi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amewapongeza kwa uamuzi wao wa kutembelea miradi inayotekelezwa na TASAF kwa Mkoa wa Mwanza.

Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwataka wanawake wa mkoa wa Mwanza kutumia fursa kubwa ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ukiwemo ule uliokamilika wa  Daraja la J.P Magufuli na miradi mingine iliyotekelezwa mkoani Mwanza waitumie kufanya biashara zao.

Kaimu Mkurugenzi wa TASAF Japhet Boaz amesema lengo la ziara ya viongozi hao ni kujionea miradi mbalimbali iliyotekelezwa na TASAF katika mkoa wa Mwanza

Kwa upande wake mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wenza wa Viongozi, Tunu Pinda ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Mwanza na TASAF makao makuu kwa utekelezaji wa miradi mingi na mikubwa na kugusa maisha ya watu wenye uhitaji.

Akizungumza na wanufaika, walimu na wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Mfano Igogwe  iliyojengwa kwa ufadhili wa TASAF, ambapo amekabidhi mitungi ya gesi 25 ya kupikia kutoka kwa wanawake wenza wa viongozi  kwa akina mama wanufaika kwa ajili ya kurahisisha shughuli zao za ujasiriamali kwa wanawake wanaofanya biashara ya kukaanga samaki na kwenye uuzaji wa vyakula.

Amesema pia mitungi hiyo pia ni sehemu ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia za kuwezesha watu kutumia nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi mazingira.

“Tunaamini kabisa mitungi hii itawasaidia kabisa katika kuboresha na kuimarisha uchumi wenu, pale TASAF wanapoanza na sisi tunaongeza na tutaendeleakuwaunga mkono,” alifafanua.

Akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Mratibu wa TASAF Manispaa ya Ilemela, Leonard Robert amesema katika awamu ya tatu ya TASAF, halmashauri ya manispaa ya Ilemela imetoa ruzuku ya zaidi ya Sh bilioni sita kuanzia mwaka 2020 hadi sasa kwa kaya maskini zaidi ya 5000.

Kwa upande wa miradi ya kupunguza umaskini, amesema halmashauri ilipokea zaidi ya Sh bilioni 2.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 46 ya maendeleo.

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Igogwe Uswege Mwakalobo amesema gharama za ujenzi wa shule hiyo zimetona na TASAF kwa kushirikiana na jamii inayoizunguka shule hiyo ikiwemo michango yao ya kushiriki kwenye ujenzi.

Aidha amesema TASAF imefadhili jumla ya miradi 12 iliyotekelezwa katika shule  ambayo imegharimu kiasi cha Sh milioni 891 na ameitaja baadhi ya  miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na vyoo sita uliogharimu Sh milioni  67.3 ujenzi wa jengo la utawala hatua ya awali ya kuezeka  Sh milioni 48.7, ujenzi wa paa hadi hatua ya kukamilika ambapo Sh milioni 72.44  na ujenzi wa maabara ambapo kiasi cha Sh milioni 68.3 kilitumika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii