Mgogoro kuhusu mahali atakapozikwa Rais wa zamani wa ZambianEdgar Lungu umechukua sura mpya baada ya Mahakama Kuu ya Afrika Kusini kusitisha mazishi yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo, Jumatano.
Familia ya Lungu ambayo imepinga ushiriki wa Rais wa sasa wa Zambia Hakainde Hichilema katika mazishi hayo imeshindwa kumzika leo Juni 25, 2025 baada ya Mahakama Kuu ya Afrika Kusini kutoa zuio la muda hadi pale kesi ya msingi iliyofunguliwa na Serikali ya Zambia itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Kesi hiyo ya msingi kuhusu maombi ya Serikali ya Zambia imepangiwa kusikilizwa tena Agosti 4, 2025.
Familia iliamua kutohamisha mazishi yake na kupanga ibada yao ya mazishi pamoja na mazishi ya faragha. Viongozi wakuu wa chama cha kisiasa cha Lungu walisafiri kwenda Afrika Kusini kuhudhuria mazishi.
Serikali ya Zambia kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wake Mulilo Kabesha iliwasilisha maombi ya dharura katika Mahakama Kuu ya Afrika Kusini na imefanikiwa kupata amri ya kusitisha mazishi ya faragha ya Rais wa zamani Lungu, yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo nchini humo.