MAMLAKA ya Mawasiliano nchini Kenya (CAK) imevitaka vyombo vya habari nchini humo kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano yaliyofanyika jijini Nairobi, ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kuanza kwa vuguvugu la vijana la Gen Z.
Maandamano hayo yameibua taharuki katika miji kadhaa huku vikosi vya usalama vikiwa vimewekwa katika maeneo muhimu.Maandamano hayo yalianza kama ishara ya upinzani dhidi ya gharama kubwa ya maisha, ambapo mwaka jana vijana walivamia bunge wakishinikiza mabadiliko ya sera za kiuchumi.
Hadi sasa, miji kama Eldoret, Nakuru, Kisii na Mombasa imeripotiwa kushuhudia maandamano huku polisi wakiongeza uwepo wao kwa ajili ya kudhibiti hali. Katika kaunti ya Uasin Gishu, hususan mjini Eldoret, polisi waliovalia sare rasmi na silaha wameonekana wakidhibiti vikundi vya waandamanaji.
Maeneo ya katikati mwa jiji yameshuhudia misuguano ya hapa na pale kati ya vijana na maafisa wa usalama. Nakuru pia imeshuhudia umati mkubwa wa vijana waliobeba mabango, wakikumbuka waathirika wa maandamano ya mwaka jana waliopoteza maisha kwa kupigwa risasi. Maandamano hayo pia yameenea katika mji wa Kisii na sehemu za Mombasa, huku vijana wakiendelea kutoa wito wa mageuzi ya kiuchumi.
Hali jijini Nairobi imeendelea kuwa tete, hasa katika Barabara ya Kenyatta ambapo makundi ya vijana wamekuwa wakikabiliana na polisi kwa saa kadhaa sasa. Ripoti zinaonesha kuwa idadi ya maafisa wa usalama imeongezwa ili kuimarisha hali ya utulivu katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Vuguvugu la Gen Z lilianza Juni 2024 nchini Kenya kufuatia maandamano makubwa ya vijana waliopinga kupanda kwa gharama ya maisha, ukosefu wa ajira na mzigo mkubwa wa kodi. Maandamano ya awali yalimalizika kwa ghasia na vifo, hali iliyosababisha tahadhari kubwa kwa serikali mwaka mmoja baadaye.
Serikali inahofia kurudiwa kwa hali hiyo, jambo lililopelekea kuamuru kusitishwa kwa matangazo ya moja kwa moja kwa lengo la kuzuia uchochezi.