Waliotemwa na Samia kuwania nafasi za ubunge katika majimbo hayo

RAIS Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi na kuhamisha viongozi mbalimbali, wakiwemo wakuu wa mikoa watano na wakuu wa wilaya 17.

 Hatua hiyo imebainisha majimbo ambayo viongozi walioachwa katika uteuzi huo wameazimia kugombea ubunge katika majimbo hayo.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda anatajwa kulitaka Jimbo la Arusha Mjini ambalo kwa sasa linashikiliwa na Mrisho Gambo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akihutubia Baraza la Madiwani la Arusha Mjini wakati wa kulivunja baraza hilo, Makonda alisikika akiwataka madiwani hao wamuombee na pale wakisikia jina lake huko nje linatajwatajwa wamuunge mkono.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba anatajwa kuingia katika kinyang’anyiro cha kulitaka Jimbo la Kigoma Kaskazini ambako mtifuano unatarajiwa kati yake na mbunge anayemaliza muda wake, Assa Makanika.

Katika uteuzi huo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye ameachwa na anahusishwa na harakati za kulitaka Jimbo la Busokelo mkoani Mbeya ambapo atapambana na mbunge anayemaliza muda wake Atupele Mwakibete.

Vilevile, miongoni mwa viongozi walioachwa katika uteuzi huo ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Dk Juma Homera ambapo taarifa zinabainisha ametia nia ya kulitaka Jimbo la Namtumbo na anatarajiwa
kuchuana na mbunge anayemaliza muda wake, Vita Kawawa, mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Rashid
Kawawa.

Aidha, uteuzi huo pia umemweka kando aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ambaye anatajwa kulinyatia Jimbo la Makambako ambako atakabana koo na mbunge anayemaliza muda wake, Deus Sanga.

Mbali na wakuu wa mikoa, taarifa zinabainisha wapo wakuu wa wilaya ambao pia wameondolewa katika nafasi zao kutokana na kutamani viti vya ubunge.

Miongoni mwao ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo ambaye anatajwa kusaka ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kagera.

Viongozi wengine walioachwa katika uteuzi huo ni wakuu wa taasisi za umma ambao pia uchunguzi unaonesha kuwa kilichowaponza ni hamu yao ya kupata jimbo nchini.

Mfano mzuri katika hili ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa ambapo taarifa zinasema hamu yake ya kulipata Jimbo la Bariadi Vijijini ndiyo sababu ya kuondolewa katika nafasi yake, ikachukuliwa na Machibya Masanja.

Panga la Rais Samia lilitembea mpaka kwa makatibu wakuu ambapo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe anatarajiwa kuwania ubunge katika Jimbo la Lushoto.

Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Profesa Shemdoe alisema ameamua kujitosa katika jimbo hilo kwa sababu
hakuna mwanasiasa mwenye hakimiliki ya jimbo lolote nchini bali ni haki ya kila Mtanzania.

Mbali na viongozi wa umma waliotonesha nia ya kugombea ubunge na udiwani, wanasiasa na wanachama wa CCM wamejitokeza mkoani Kagera kutafuta majimbo ni Mwalimu Josias Charles (Ngara), Simon Patrick (Muleba Kusini), Projestus Tegamaisho (Missenyi), Faris Buruhani (Bukoba Vijijini) na Almasou Kamala (Bukoba Mjini).

Katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka Juni 23, Rais Samia amemteua Balozi Simon Sirro kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma akichukua nafasi ya Thobias Andengenye huku Kheri James akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuchukua nafasi ya Peter Serukamba.

Aidha, Rais Samia amemteua Mboni Mhita kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akichukua nafasi ya Anamringi Macha ambaye amehamishiwa Simiyu huku Beno Malisa akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya akichukua nafasi Dk Juma Homera.

Katika uteuzi huo, Rais Samia alimteua Jabiri Makame kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe akichukua nafasi ya Daniel Chongolo huku Agnes Meena akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi akichukua nafasi ya Profesa Riziki Shemdoe.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameteua na kuhamisha makatibu tawala wa mikoa ambapo amemteua Abdul Mhinte kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam na Dk Frank Hawasi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe.

Kwa mujibu wa Dk Kusiluka, Rais Samia amemhamisha Rashid Mchata kutoka Mkoa wa Pwani kwenda kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga na Pili Mnyema kutoka Mkoa wa Tanga kwenda kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani.

Miongoni mwa waliohamishwa pia yumo Dk Hussein Omar kutoka Wizara ya Kilimo kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Rais Samia pia alifanya uteuzi wa Naibu Makatibu Wakuu ambapo Profesa Peter Msoffe ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya mazingira huku Athumani Kilundumya akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya mazao na usalama wa chakula.

Kwa upande wa wakuu wa wilaya, Rais Samia alifanya uhamisho na uteuzi ambapo Solomon Itunda amehamishwa kutoka Wilaya ya Songwe kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya.

Taarifa hiyo pia imeonesha kuwa Japhari Mghamba amehamishwa kutoka Wilaya ya Handeni kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Gairo na Amir Mkalipa amehamishwa kutoka Wilaya ya Arumeru kwenda kuwa Mkuu wa
Wilaya ya llemela.

Wakuu wapya wa wilaya walioteuliwa na wilaya walikopangiwa ni Estomin Kyando (Kilolo), Ayubu Sebabile (Muheza), Thecla Mkuchika (Butiama), Angelina Lubela (Serengeti), Maulid Dotto (Mvomero) na Rukia Zuberi (Mwanga). Wengine ni Mwinyi Mwinyi (Arumeru), Jubilete Lauwo (Magu), Mikaya Dalmia (Kigamboni), Thomas
Myinga (Sikonge), Gloriana Kimath (Monduli), Upendo Wella (Tabora), Denis Masanja (Tunduru), Fadhil Nkurlu (Songwe), Benjamin Sitta (Iringa) Salum Nyamwese (Handeni) na Frank Mkinda (Kahama).

Uteuzi mwingine ni wa Makatibu Tawala wa Wilaya ambapo Mwanamwaya Kombo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala (Mkinga), Kassim Kirondomara (Biharamulo), Thobias Abwaro (Babati), Asycritus Egaruk (Meatu), Nyakaji Mashauri (Kilolo), Mustapha Kimomwe (Rufiji) na Milama Masiko (Serengeti).

Wengine katika uteuzi huo ni Mpampalika Mpampalika (Mwanga), Richard Mwalingo (Mtwara), Zuberi
Zuberi (Magu), Angela Mono (Tanga), Mamndolwa Gembe (Same), Sabina Mwajeka (Momba) Sosthenes Chakupanyuka (Kaliua) na Adestino Mwilinge (Mbogwe).

Kwa upande wa wakurugenzi wa halmashauri, Rais Samia ameteua na kuhamisha ambapo amemhamisha Justice Kijazi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwenda Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Zaina Mlawa amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kwenda Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Kwa upande mwingine Rais Samia alifanya uteuzi wa wakurugenzi watendaji wa halmashauri ambapo Raymond Mweli (Mbarali), Adelina Mfikwa (Bukombe), Iddi Ndabona (Bariadi), Hamisi Idd (Busega), Mwarami Seif (Nzega) na Newaho Mkisi (Meatu).

Wengine ni Zainab Mgomi (Nanyamba), Dk John Pima (Manispaa ya Tabora), Albina Mtumbuka (Bahi), Paulo Faty (Mvomero) Shabani Kabelwa (Kaliua) na Vicent Mbua (Ukerewe).

Rais Samia pia alifanya uteuzi wa mkuu wa taasisi ambapo Machibya Masanja ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) akichukua nafasi ya Masanja Kadogosa.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga ilisema uapisho wa Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Naibu Makatibu Wakuu wateule utafanyika kwa tarehe itakayopangwa baadaye.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii