Majaliwa yatangaza taasisi za umma kujiunga na mfumo wa kielektronik kuanzia juni 23 hadi julai 30

JUZI Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa maagizo saba kwa taasisi za umma na watumishi wa umma kuhusu mifumo kusomana akilenga dhamira ya serikali ya kuimarisha utendaji kazi nchini.

Ametangaza kuanzia Juni 23 hadi Julai 30 mwaka huu, taasisi za umma zijiunge na mfumo wa kielektroniki utakaowezesha mifumo ya serikali kuwasiliana (GovESB).

Majaliwa alitoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati wa kuzindua mifumo ya kielektroniki ya utoaji huduma kwenye maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma.

Kama ambavyo serikali inaamini, na sisi tunaamini kwamba hatua hiyo pamoja na mambo mengine itasaidia kudhibiti rushwa na kuimarisha ulinzi wa taarifa za serikali.

Tunasema hivyo kwa sababu maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa taasisi za umma kuunga mifumo yao na mfumo huo uliofanyiwa kazi na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni muhimu kwa kuwa unalenga kuzuia mianya ya rushwa, kuondoa uzembe wa makosa ya kibinadamu na kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa umma.

Ni wazi mfumo huu usio na gharama kujiunga, umelenga kurahisisha utendaji kwa kupunguza urasimu, vishawishi na kuimarisha ulinzi wa taarifa za serikali.

Ili kuleta ufanisi katika hili, taasisi zote za umma zenye mifumo na zinazoendelea kubuni mifumo zinapaswa kuhakikisha mifumo hiyo inasomana na inaweza kubadilishana taarifa kupitia GOvESB ili kuboresha huduma za serikali kwa jamii.

Kama alivyoelekeza Majaliwa, e-GA nao wanapaswa kuhakikisha mifumo iliyounganishwa inaendelea kubadilishana taarifa na kila anayeingia kuitumia ajiridhishe kwa kuwasiliana na wengine walioko katika mfumo huo.

Aidha, wakuu wa taasisi hawajasahaulika, wameagizwa waandaliwe utaratibu wa uelewa wa mifumo muhimu ya kiutumishi iliyopo ili malengo ya kuwepo mfumo huo yafikiwe.

Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alinukuliwa akisema Tanzania inatambuliwa kimataifa kwa ukomavu wa matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma, hivyo mfumo huo ni udhihirisho wa hayo na utekelezaji wa maono ya viongozi wa kitaifa hasa Rais Samia.

Maagizo ya Majaliwa na kauli ya Simbachawene zinaongeza msukumo wa ulazima wa taasisi kujiunga na mfumo bila kusubiri makaripio au kuwajibishwa kwa lazima kwani mpaka sasa mifumo 223 kutoka kwenye taasisi 185 pekee ndiyo imeunganishwa na kusomana.

Tunaunga mkono maagizo ya Waziri Mkuu na kwamba tarehe ya mwisho wa kujiunga na mfumo kwa taasisi za umma ikifika, taasisi ambazo hazijajiunga zijieleze. Jambo hili ni jema, taasisi za umma zilitendee haki.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii