Wadau wa siasa watabiri ongezeko la wabunge wapya bunge lijalo

WADAU wa siasa wamesema bunge lijalo linaweza kuwa na wabunge wengi wapya kutokana na wabunge wanaomaliza muda wao wengi kutotatua changamoto za wananchi kwenye majimbo yao.

Akizungumza na waandishi wa habari mchambuzi wa masuala ya siasa na Jamii, Abdulkarim Atiki amesema bunge limetimiza wajibu wake kitaifa kama mhimili wa pili wa dola, lakini kwa wabunge mmoja mmoja katika majimbo yao ni wachache waliomudu kutatua changamoto za wananchi na kuwasemea.

Ni ishara ya kuwa wengi hawatarejea kwenye bunge lijalo kwa sababu waliingia bungeni kwa maslahi yao binafsi na si kwa maslahi ya wananchi waliowachagua kuingia katika bunge hilo hivyo kutokana na marekebisho ya sheria za uchaguzi ikiwemo ya Sheria ya Tume ya Uchaguzi, vyama vya upinzani vikijipanga watapata wabunge na bunge litachangamka

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema mbunge anavyoapa anakuwa mtiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maana ya kwamba wajibu wake mkubwa ni kusimamia na kuishauri serikali kwa niaba ya wananchi kwa sababu ndio waliowachagua na si vinginevyo.

Mkazi wa Dar es Salaam, Mathew William alisema wapo baadhi ya wabunge walioingia kuangalia maslahi binafsi badala ya kupigania maslahi ya wananchi waliowachagua.

Beniventura Malongo alisema miaka mitano ya bunge linalohitimishwa keshokutwa yamefanyika mambo mazuri ambayo yanawagusa wananchi ikiwemo masuala ya maji, afya na elimu ,Wapo wabunge waliogusa mahitaji ya wananchi, lakini wapo wawakilishi wetu walibeba nafasi zao zaidi, walijizungumzia zaidi wenyewe kuliko tuliowatuma kutuwakilisha na pale waliporudi katika majimbo yetu hawakupata nafasi ya kuitisha mikutano na wananchi kuwapa mrejesho,” alisema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii