Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dustan Kitandula alisema hayo bungeni Dodoma juni 23 alipoeleza mafanikio ya sekta ya utalii wakati akichangia taarifa ya hali ya uchumi, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2025/2026 na mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kitandula alisema kwa sasa Tanzania ina simba takribani 17,000, nyati 225,000 na chui 20,000, Tanzania ilikuwa na faru 163 lakini sasa wapo 263 sawa na ongezeko la asilimia 61.
Kitandula alisema wakati wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kumekuwa na ongezeko kubwa la utalii kutoka milioni 1.7 mwaka 2021 hadi milioni 5.3 mwaka 2024.
Alisema hilo ni ongezeko la asilimia 107.2 zaidi ya maagizo ya kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025.
“Kwa ongezeko hili wenzetu duniani Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii limeitambua Tanzania ni kinara wa utalii katika Afrika kwa ongezeko la idadi ya watalii,” alisema.
Aliongeza: “Ukuaji ambao umepatikana ni asilimia 48 ikilinganishwa na idadi ya watalii waliokuwa wanaingia nchini wakati ule wa kipindi cha Covid-19”.
Kitandula alisema mapato yanayotokana na shughuli za utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi Dola bilioni 3.9 mwaka jana, sawa na ongezeko la asilimia 200 kwa watalii wanaotoka nje.
Aliwaeleza wabunge mapato yanayotokana na utalii wa ndani yameongezeka kutoka Sh bilioni 46.3 mwaka 2021 hadi Sh bilioni 209.8 mwaka jana, sawa na ongezeko la asilimia 353.1.
“Hongera sana kwa Watanzania kwa kuitikia mwito huu, mafanikio haya ya ongezeko la watalii yameifanya Tanzania kushika nafasi ya tisa duniani na nafasi ya tatu Afrika kwa ongezeko la mapato katika sekta ya utalii,” alisema Kitandula.
Alisema mwaka jana Tanzania ilipata tuzo ya eneo linaloongoza kwa utalii wa safari duniani na pia ilipata tuzo ya eneo linalovutia zaidi kwa utalii Afrika.
“Hifadhi yetu ya Serengeti ikapata tuzo ya kuwa hifadhi bora duniani na hii imekwenda kwa miaka sita mfululizo. Mlima Kilimanjaro ulipata tuzo ya kuwa kivutio bora cha utalii Afrika…” alisema Kitandula na akaongeza kuwa miaka sita mfululizo Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) imepata tuzo ya kutoa huduma kwa kiwango cha kimataifa.
Alisema Tanzania imeimarisha biashara ya mazao ya misitu na mwaka jana ilipata mapato Sh bilioni 458.4 kwa kuuza mazao hayo.
Kitandula alisema mwaka jana Tanzania na China zilisaini makubaliano ya soko la asali inayozalishwa nchini na kwa mwaka nchi hiyo inahitaji tani milioni 38.