Abbas Tarimba atoa yake ya moyoni kumtetea Rais –

MBUNGE wa Jimbo la Kinondoni, Abbas Tarimba, amesema atasimamia ukweli kwa kueleza na kutetea mazuri yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Tarimba amesema tangu Rais Samia aingie madarakani, amekuwa kinara wa mageuzi ya maendeleo nchini na kwamba hatasita kupambana na yeyote anayemkosoa kiongozi huyo bila hoja za msingi.

“Ndiyo maana nilijitosa, nikasema atakayemtingisha Rais nami nitamtingisha. Bila shaka nimekuwa nikifanya hivyo ndani na nje ya Bunge,” alisema Tarimba.

Mbunge huyo alibainisha kuwa malipo makubwa wanayopaswa kumpa Rais Samia ni kuhakikisha anaendelea kuaminiwa na wananchi kwa kumpigia kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu ujao.

Katika kipindi cha miaka mitano ya uwakilishi wake, Tarimba amesema jimbo la Kinondoni limeshuhudia mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu na miundombinu.

Ameeleza kuwa kupitia mfuko wa jimbo na juhudi zake binafsi, wamefanikiwa kujenga vituo vya afya, kuboresha barabara, na kusaidia shule kupitia michango ya maendeleo.

Mbali na hilo, Tarimba amesema amejitolea kutoa bima za afya kwa zaidi ya wananchi 1,300 jimboni kwake, akisisitiza kuwa afya bora ni msingi wa maendeleo ya jamii.

Kwa kuhitimisha, Tarimba amesema yuko tayari kuendelea kulitumikia jimbo hilo kwa awamu nyingine, endapo wananchi watamrejesha tena kwa imani yao.



Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii