Majaliwa yatoa maagizo 7 kwa taasisi na watumishi wa umma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo saba kwa taasisi za umma na watumishi wa umma kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi.

Ametangaza kuanzia jana hadi Julai 30 mwaka huu taasisi za umma zijiunge na mfumo wa kielektroni utakaowezesha mifumo ya serikali kuwasiliana (GovESB).

Hatua hiyo pamoja na mambo mengine itasaidia kudhibiti rushwa na kuimarisha ulinzi wa taarifa za serikali.

Majaliwa alitoa maelekezo hayo jana jijini Dodoma wakati wa kuzindua mifumo ya kieletroniki ya utoaji huduma kwenye maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma.

Msisitizo uliotolewa na Rais (Samia Suluhu Hassan) kuwa pindi e-GA (Mamlaka ya Serikali Mtandao) ikikamilisha kazi hiyo taasisi ziunge mifumo yao, lakini taasisi zilizojiunga ni chache ikilinganisha na idadi ya taasisi tulizonazo ndani ya serikali.

Alisema kwa kutumia mfumo huo, serikali imelenga kupunguza vishawishi na kuimarisha ulinzi wa taarifa za serikali.

Mpaka juni 23  jumla ya mifumo 223 kutoka kwenye taasisi 185 imeunganishwa na kusomana.

Aidha, Majaliwa amezitaka taasisi zote za umma zenye mifumo na zinazoendelea kubuni mifumo zihakikishe mifumo hiyo inasomana na inaweza kubadilishana taarifa kupitia mfumo huu wa GOvESB ili kwenda kwenye gurudumu moja la kuboresha huduma ndani ya serikali.

Pia aliielekeza eGA kuhakikisha mifumo iliyounganishwa inaendelea kubadilishana taarifa, lakini kila anayeingia ajiridhishe anaweza kuwasiliana na wengine wote waliko huko ndani.

Majaliwa pia ameelekeza taasisi zote za umma ziendelee kutenga bajeti ya kutosha ili kushiriki kikamilifu bila kukosa katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kila mwaka.

Pia alielekeza kuimarishwa mikakati ya kuhamasisha Wananchi kujenga utamaduni wa kutumia fursa za uwepo wa maadhimisho kama haya ili wajitokeze na kunufaika na huduma mbalimbali.

Aliwaagiza watumishi wa umma kuzingatie miiko na maadili ya utumishi wa umma na kuzingatia sera, sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo ya serikali wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.

Majaliwa pia aliwaagiza wakuu wa taasisi nchini waandaliwe utaratibu wa uelewa wa mifumo muhimu ya kiutumishi iliyopo.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema Tanzania inatambuliwa kimataifa kwa ukomavu wa matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za serikali na ushirikishwaji wa wananchi.

Pia alisema wizara yake kupitia e-GA imetekeleza maono na maelekezo ya viongozi wa nchi kwa kujenga mfumo wa GovESB.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii