Waziri wa Nchin Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema tafiti
zinaonesha samaki na dagaa wanaopatikana katika Ziwa Victoria
hawajaathirika kwa zebaki.
Amesema hayo bungeni jijinin Dodoma
wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Juliana Masaburi
aliyetaka kufahamu iwapo Serikali imefanya utafiti kuhusu samaki hao
iwapo wameathiriwa na kemikali hiyo kama inavyodaiwa.
Dkt. Jafo
alisema kuwa wataalamu wanaendelea kuhakikisha matumizi mbalimbali ya
kemikali hiyo katika maeneo ya Kanda ya Ziwa yanadhibitiwa huku
akiwataka waendelee kuzingatia masuala mahsusi ya kimazingira ili
kulinda nchi yetu.
Pia, akijibu swali kuhusu udhibiti wa uchafuzi
pembezoni mwa Ziwa Victoria ambao unapunguza samaki kuzaliana hivyo
shughuli za uvuvi kudorora, waziri huyo alisema Serikali imeandaa
Kanuni, Miongozo na kuhakikisha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM)
inafanyika kwa miradi ya maendeleo iliyopo na inayotarajiwa kufanyika
pembezoni mwa ziwa hilo.
Aliongeza kuwa imeandaliwa mikakati
pamoja na kuendelea kutekeleza katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki
kwa ajili ya kubebea bidhaa ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ikichangia
uchafuzi pembezoni mwa Ziwa Victoria.
Hata hivyo, Dkt. Jafo
alibainisha kuwa uchafuzi wa mazingira unaofanyika pembezoni mwa ziwa
unatokana na shughuli za kibinadamu zisizozingatia hifadhi ya mazingira
zikiwemo utiririshaji wa majitaka kutoka katika maeneo ya makazi pamoja
utupaji wa taka ngumu kutoka majumbani na viwandani.
Alitaja
shughuli zingine kuwa ni kilimo kisicho endelevu kinachosababisha
uchafuzi wa maji kutokana na kuongezeka kwa tabaki (segments) na
matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu na mbolea za viwandani na uchimbaji
wa madini usio endelevu.