Marekani yakanusha kusitisha silaha kwenda Ukraine

MAAFISA wa serikali ya Marekani wametupilia mbali taarifa ya awali kutoka Ikulu ya White House inayodai kuwa Washington inazuia usafirishaji wa baadhi ya silaha kwenda Ukraine, wakati ambapo taifa hilo linaendelea kukabiliwa na mashambulizi makali kutoka kwa majeshi ya Urusi.

Akizungumza na waandishi wa habari Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Sean Parnell, amesema wizara yake bado inaendelea kutoa ushauri kwa Rais Donald Trump kuhusu njia mwafaka za kuiunga mkono Ukraine kijeshi, huku akisisitiza kuwa hatua yoyote inayochukuliwa inalenga kufanikisha dhamira ya Marekani ya kumaliza vita hivyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Tammy Bruce, naye alifafanua kuwa tangazo la White House halikumaanisha kusitishwa kwa usafirishaji wa silaha kwa jumla, bali lilihusu tukio mahususi, pasipo kuweka wazi ni aina gani ya silaha zinazozuiwa.

Siku ya Jumanne, White House ilitangaza kusitishwa kwa baadhi ya silaha ambazo awali ziliahidiwa na utawala wa Rais wa zamani, Joe Biden, lakini haikutaja undani wa silaha hizo wala sababu kamili ya uamuzi huo.

Katika hotuba yake jana jioni, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alisema maafisa wa serikali yake wanaendelea na mazungumzo na wenzao wa Marekani kuhusiana na suala hilo, wakilenga kutafuta suluhisho la haraka.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii