BUNGE la Venezuela linaloungwa mkono na serikali limemtangaza Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Volker Turk kuwa mtu asiyetakiwa nchini humo.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya ripoti ya hivi karibuni ya ofisi ya Turk kuelezea kuzorota kwa hali ya haki za binadamu nchini humo, ikiwa ni pamoja na vizuizi kiholela, ukiukwaji wa taratibu na kutoweka kwa watu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Kamishna Turk aliishutumu serikali ya Rais Nicolas Maduro kwa kukiuka haki za msingi, hali iliyochochea hasira ya wabunge wanaomuunga mkono kiongozi huyo.
Spika wa Bunge, Jorge Rodriguez ambaye ni mshirika wa karibu wa Maduro, aliitaka serikali kusitisha uhusiano rasmi na ofisi ya Turk, ambayo imekuwa na uwakilishi nchini humo tangu mwaka 2019.
Kwa upande wake, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Venezuela imeitaja ripoti hiyo kama uchokozi dhidi ya taifa hilo.