Siku moja baada ya Chama Cha Alliance Democratic For Change (ADC) kumpata mgombea urais wa Tanzania na Zanzibar, kada wa chama hicho na aliyewahi kuwa Mbunge wa Mwibara mkoani Mara, Mutamwega Mgaywa amekusudia kukata rufaa kwenda Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, kupinga mchakato huo.
Msingi wa kuchukua uamuzi huo ni kutaka haki itendeke dhidi ya kitendo anachodai cha kihuni kilichofanywa na uongozi wa chama hicho kumuengua kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya kugombea urais wa Tanzania, kwa kunyofoa baadhi ya taarifa zake muhimu zilizojazwa kwa ufasaha na kuwekwa nyingine asizozitambua.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Juni 29, 2025, ukiambatana na mkutano mkuu maalumu, wajumbe wa chama hicho walimchagua, Wilson Elias kuwa ndiyo mgombea urais wa chama hicho kwa upande wa Tanzania bara huku mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Hamad Rashid akichaguliwa kugombea urais upande wa visiwani.
Mgaywa aliondolewa kwenye ukumbi wa mkutano huo kinguvu kwa kile kilichoelezwa hakuwa sehemu ya wajumbe halali licha ya kuwa ni mtia nia wa nafasi ya kuomba ridhaa ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.