Aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga amelaani vikali wito wa waziri wa usalama nchini Kenya Kipchumba Murkomen kwa polisi kuwafyatulia risasi watu watakaojaribu kukaribia vituo vya polisi na kuongeza kuwa anayewataka polisi kufyatulia raia risasi anapaswa kulaaniwa vikali.
Hatua hii inatajwa kuwa kama ukosoaji wa nadra kwa utawala wa Rais William Ruto hasa kwasababu chama cha Bwana Odinga kina wanachama wake watano wanaohudumu katika baraza la mawaziri katika mpango wa serikali ya muungano a maarufu ''broad based government.''
Waziri Murkomen alisema alitoa agizo hilo baada ya vituo vya polisi kushambuliwa wakati wa maandamano siku ya Jumatano, lakini matamshi yake yalitafsiriwa vibaya.
Murkomen alisema kauli zake ziliambatana na Kifungu B(1) cha Sheria ya Huduma ya Polisi ya Kitaifa, ambayo inaruhusu maafisa kutumia bunduki kujilinda au kuwalinda wengine dhidi ya vitisho vya kifo au majeraha mabaya.
Odinga pia alizungumzia matukio ya maandamano ya Juni 25, ambapo watu kadhaa walipoteza maisha huku akilaani wahalifu walioingilia maandamano hayo na kupora na kuharibu mali ya umma.
Aidha alitoa wito wa kuwepo kwa mazungumzo ya kitaifa, akiwataka wananchi na viongozi kufanya mazungumzo yenye maana ili kuandaa njia ya umoja nchini.