Rais wa Kenya William Ruto amepuuzilia mbali wito ambao umekuwa ukitolewa na waandamanaji na viongozi wa upinzani kumtaka ajiuzulu na kuwapa changamoto ya kutoa mpango mbadala ufaao badala ya kuchochea ghasia na machafuko nchini.
Akizungumza huku kukiwa na ongezeko la mvutano wa kisiasa na maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali yake, Bw Ruto alipuuzilia mbali wito “Ruto lazima aondoke”, ambao pia umekuwa ukitolewa kwenye mitandao ya kijamii kupitia #RutoMustGo na kusema hayo ni maneno matupu isipokuwa pale yatakapoambatana na mkakati halali na wa kujenga.
“Ikiwa ni suala la masharti, Katiba tayari imeshatatua na kusuluhisha suala la ukomo wa muda.
Unaweza kuwa wa muhula mmoja au miwili… Huwezi kuwa na zaidi ya hayo. Kwa hivyo ni nini shauku hii kuhusu masharti?” Rais alihoji.
Aidha amesema “Ikiwa ni Ruto lazima aende, basi niambie jinsi unavyotaka niende. Unamaanisha nini unaposema Ruto lazima aende? Niendeje? Kwa sababu tuna katiba”, alisisitiza rais huyo wa Kenya.