Gavana motoni kwa kuwadhalilisha wanawake wa Taita

WANAWAKE katika Kaunti ya Taita Taveta wamemtaka Gavana Andrew Mwadime kuomba msamaha kwa matamshi ya kuwadhalilisha.

Hii ni baada ya Gavana Mwadime kudai kuwa wanawake warefu katika kaunti hiyo wameolewa nje ya gatuzi na kwamba waliosalia ni wafupi ambao ni wasumbufu.

Gavana alitoa matashi hayo wiki jana wakati wa kikao cha maafisa wa serikali ya kaunti na Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Fedha za Umma (CPAC) inayoongozwa na Seneta Moses Kajwang’.

Alipoulizwa na Seneta Kajwang’ ikiwa wanawake wafupi si warembo, Bw Mwadime alisema wao huwa wana ugomvi na husumbua.

Sasa wanawake wakiongozwa na shirika la Sauti ya Wanawake wanasema gavana aliwakosea heshima wanawake wote wa eneo hilo kwa kudai wale wafupi wanapenda ugomvi.

Mwenyekiti wa shirika hilo Bi Lydia Mwamberi alipuuzilia mbali madai kuwa Gavana alikuwa akifanya mzaha alipotoa matamshi hayo, akisema wanawake kote vijijini wanalalamika kwamba aliwadharau.

Bi Mwamberi alisema walishangazwa na hatua ya gavana kudhalilisha wanawake mbele ya Seneti badala ya kujadili kuhusu masuala ya maendeleo na changamoto zinazokumba kaunti yao.

Aliapa kuwa iwapo Gavana Mwadime hataomba msamaha basi wanawake wa eneo hilo wataandamana hadi atakapotoa radhi hiyo.

Ni msimamo ulioshikiliwa pia na Bi Makrina Mwamburi akisema kuwa walighadhabishwa na matamshi ya kiongozi wao na kwamba yameshusha hadhi ya wanawake eneo hilo.

Naye Bi Mary Sau alishangaa kwa nini Bw Mwadime bado anasita kuomba msamaha.

“Gavana ana mke na pia baadhi ya wafanyakazi wake ni wafupi. Matamshi hayo yametukasirisha sana. Asipoomba msamaha tutamwadhibu debeni katika uchaguzi mkuu ujao,” akasema.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii