ALIYEKUWA Mbunge wa Iringa Mjini kwa miaka 10, Mchungaji Peter Msigwa, amechukua fomu kuwania ubunge Iringa Mjini—safari hii akitokea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ametangaza dhamira yake ya dhati ya kuliongoza upya jimbo hilo, akiahidi mapambano dhidi ya umasikini na kuhakikisha mji huo wa kihistoria unapata sauti kubwa kitaifa na kimataifa.
Msigwa alikabidhiwa fomu za kugombea ubunge katika ofisi za CCM Wilaya ya Iringa Mjini na Katibu wa chama hicho, Hassan Makoba, huku akieleza kwa msisitizo kuwa wakati wa mabadiliko ya kweli kwa Iringa umefika.
“Ninauchukia umasikini. Nitashirikiana na wananchi wa Iringa Mjini kuendeleza kazi kubwa inayofanywa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kupambana na umasikini.”
Alisema anataka kurejea kwenye siasa za uwakilishi akiwa na dhamira ya kweli na uzalendo wa kuitumikia nchi, chama, na wananchi wake.
Kwa Msigwa, alisema ubunge si fursa ya kutafuta madaraka, bali majukumu ya kuwasemea wananchi na kusaidia jamii kufikia maendeleo ya kweli.
“Mji wetu una vibe, yaani mzuka wa kipekee wa mabadiliko. Tunahitaji Iringa isikike, iwe kwenye ramani ya uwekezaji, utalii na maendeleo ya kijamii. Nataka Iringa iwe injini ya mageuzi ya kimaendeleo.”
Akitaja maeneo manne muhimu ya uwakilishi wa mbunge, Msigwa alisema atakuwa sauti ya watu, msimamizi wa serikali, muwakilishi wa chama, na mzalendo wa taifa lake.
Aidha, aliwahakikishia wanachama wa CCM kuwa atashirikiana nao kujenga chama imara, akiamini kuwa maendeleo yaliyofanywa na Rais Dk Samia ni msingi thabiti wa ushindi wa kishindo kwa CCM Iringa Mjini.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini alikumbusha kuwa mchakato huo bado haujaruhusu kampeni na kuwa kila mgombea anapaswa kufuata taratibu za kichama kwa umakini na utii mkubwa ili kuepuka jina lake kuenguliwa.
“Kupokea fomu si ruhusa ya kuanza kampeni. Ni muda wa kutafakari, kujiandaa na kujaza fomu kwa umakini. Kuvunja taratibu ni kujiondoa mwenyewe kwenye mchakato.”
Kwa kurejea kwake katika siasa akiwa CCM, Msigwa anazua mjadala mpya katika ulingo wa siasa Iringa Mjini. Je, atarejea bungeni kwa mara nyingine? Majibu yatapatikana Oktoba, lakini kwa sasa, kishindo chake kimesikika.